Post Top Ad

Post Top Ad

Saturday, June 5, 2021

 Semina ya siku 30 ( Christ For All People Church- Mbeya ).

KUYASHUGHULIKIA MALANGO YA KIROHO YANAYOGUSA MFUMO WAKO WA MAISHA YA KILA SIKU.

         Day 6 ya Semina.

Senior Pastor Samwel Kibiriti.

Asifiwe Yesu Kristo mwana wa Mungu karibu katika semina ya siku ya leo tunaendelea kujifunza kuhusu lango la nchi.

KUPAMBANA NA LANGO LA NCHI UNAYOISHI ( B ).

Mathayo 12:40  Nahumu 3:13  Yona 1:8

Katika semina ya jana tulijifunza swali la kwanza kuhusu Nchi leo tuangalie swali lingine;

            SWALI LA PILI:

( 2 ) Je katika nchi kuna madhabahu za mungu yupi?.

Waamuzi 6:25-26

Kila nchi unayoiona duniani iko na madhabahu mbalimbali zilizomo ndani yake na madhabahu zilizomo ndani ya nchi zinahusika kwa asilimia kubwa kuikamata nchi na kuyakamata maisha ya nyie wananchi mnaoishi katika hiyo nchi. Ukifuatilia nchi nyingi utaziona zimejengwa madhabahu za miungu wala sio madhabahu za Mungu aliye hai katika Yesu Kristo, na hizo madhabahu za miungu zinawatesa wananchi kiroho wa hiyo nchi hata kama hamjui.

Madhabahu za nchi nyingi unaziona zimejengwa katika barabara za mikoa kwenye maeneo ya Round About pia katika ofisi za wakuu wa mikoa na wilaya ziko madhabahu zilizojengwa na kusimamishwa huko, pia katika milima ziko madhabahu na katika majumba ya makumbusho kuna madhabahu zimewekwa ndani ya hizo makumbusho n.k na madhabahu hizo za miungu nyingi zinamfano wa sanamu lakini katika ulimwengu wa roho sio sanamu bali ni madhabahu kabisa za miungu na watu hufanya mambo ya kiibada za miungu maeneo hayo.

        TAFAKARI MASWALI HAYA MOYONI MWAKO:

( A ) Viongozi katika nchi yenu wanaziabudu madhabahu za mungu yupi?.

( 1Wafalme 12:20; 25-30 ) ( 2Wafalme 13:1-6; 21:1-7 ) ( 2Wafalme 22:1-2 ).

Nataka nikuulize swali hili viongozi mbalimbali katika nchi yenu kutoka ngazi za juu hadi ngazi za chini wanaziabudu madhabahu za mungu yupi? Mungu katika Yesu Kristo au miungu? Asilimia kubwa sana za viongozi waliomo ndani ya nchi hawaabudu katika madhabahu ya Mungu katika Yesu Kristo bali huabudu katika madhabahu za miungu, na kitendo hicho cha viongozi wenu wa nchi kuabudu kwenye madhabahu za miungu husababisha hizo madhabahu za miungu zihusike na nchi yenu na maisha ya nyie wananchi mnaoishi katika nchi.

Hivyo unatakiwa kumuomba sana Mungu aigeuze mioyo ya viongozi wako isiwe inaabudu miungu bali iwe inamuabudu yeye Mungu ili nchi yenu na maisha yenu yasiweze kushikiliwa na madhabahu za miungu.

( B ) Je ni roho gani zinazotoka kwenye madhabahu za nchi yenu?.

Ufunuo 8:1-3; 14:18

🔴 Kila madhabahu ziko na roho sasa swali linakuja katika nchi unayoishi hizo madhabahu za nchi yenu zimebeba roho za aina gani? Nataka ujue kwamba roho zilizobebwa ndani ya madhabahu za nchi zinahusika na maisha yenu ya kila siku katika nchi hivyo kama madhabahu za nchi yenu zimebeba roho za giza ujue kwamba nchi itakuwa imefungwa na roho za giza na maisha yenu wananchi mtakuwa mnateswa na roho hizo za giza kwenye maisha yenu.

Hakikisha kwamba unaingia kwenye maombi kuyafungua maisha yako na maisha ya familia yako/yenu yaliyofungwa kwenye madhabahu za nchi na hizo roho za madhabahu, usipofanya hivyo utaendelea kuteseka katika nchi kutokana na hizo roho zilizomo ndani ya madhabahu za nchi yenu kiroho.

( C ) Madhabahu zilizomo ndani ya nchi yenu zinaongea nini rohoni kuhusu nchi yenu na maisha yenu?.

Ufunuo 16:7; 9:13-14  1Wafalme 13:1-3

🔵 Biblia iko wazi kwamba madhabahu zinaongea sasa nakuuliza swali hizo madhabahu zilizoko ndani ya nchi yenu zinaongea nini rohoni? Kuna mambo mengi yasiyofaa ambayo kila siku yanatamkwa kwenye hizo madhabahu za nchi yenu ndio maana unakuta kwenye ulimwengu wa roho mambo yanakuwa magumu sana kwako kutokana na sauti ambazo zinatoka kwenye madhabahu zilizomo ndani ya nchi yenu.

Hakikisha unaingia kwenye maombi na kupambana na madhabahu za nchi kisha funga kila sauti na maneno yasiyofaa yanayotoka kwenye madhabahu za nchi yenu za miungu kwasababu usipofanya maombi ya kuzinyamazisha hizo madhabahu hali yako ya kiroho haiwezi kukaa sawa. Pia jiungamanishe na madhabahu ya Mungu ili isimame pamoja nawe katika maisha yako ya kila siku.

( D ) Madhabahu zilizomo ndani ya nchi yenu je haziwali watu wake wa nchi?.

Hesabu 13:32

Kuna madhabahu ambazo zimo ndani ya nchi zinazokula watu wake waliomo ndani ya nchi, ndio maana kuna vifo ambavyo hutokea katika nchi vinavyokosa majibu ya kibinadamu na vifo hivyo hutokea katika ajali, magonjwa, ugomvi n.k na chanzo cha vifo hivyo huwa madhabahu za miungu za nchi kumbe zimeinuka na kula watu. Sio kila vifo unavyoviona katika nchi yenu ni mapenzi ya Mungu hapana vingi tu ni matokeo ya kuwepo madhabahu za miungu katika nchi na ndizo zinazokula watu katika nchi.

🔶 Hakikisha kwamba unapambana na madhabahu za nchi na kuyafungua maisha yako na maisha yenu kila siku.

✔️ Kwa leo tafakari swali hili na kufanyia kazi kwa maombi kila siku na siku ya kesho tutaona swali la tatu kuhusu lango la nchi. Nakuomba unisaidie kuwashirikisha wengine masomo haya kila siku ya Semina ili nao wapokee Maarifa na kupokea majibu toka kwa Mungu.

Kwa mawasiliano nami utanipata kwa namba hizi, pia unaweza kumshukuru Mungu kwa sadaka zako kupitia Semina hii.

Vodacom M-PESA +255 765 867574 ( WhatsApp ).

Airtel Money +255 785 855785

Tigo Pesa +255 673 784197

Kwa Email address ni Pastorkibiriti@gmail.com



Mimi ni Mwalimu wa Neno la Mungu la Maarifa

          Samwel Kibiriti.

Mei 20, 2021

Mbeya Tanzania.

@Kibiriti2021

Tukutane siku ya kesho ya semina.

No comments:

Post a Comment

Featured Post

JINSI MISINGI YA VIZAZI INAVYOWEZA KUKAMATA MAISHA YAKO.

Fahamu kwamba misingi ni chanzo au asili au chimbuko la mtu. Na msingi wako wa vizazi unatokana na ukoo wako na kabila lako.      ...