Semina ya siku 30 ( Christ For All People Church- Mbeya ).
KUYASHUGHULIKIA MALANGO YA KIROHO YANAYOGUSA MFUMO WAKO WA MAISHA YA KILA SIKU.
Day 7 ya Semina.
Senior Pastor Samwel Kibiriti.
Bwana Yesu Kristo asifiwe karibu mwana wa Mungu tuendelee na semina yetu.
KUPAMBANA NA LANGO LA NCHI UNAYOISHI ( C ).
Mathayo 12:40 Nahumu 3:13 Yona 1:8
Katika semina ya siku ya jana tuliangalia swali la Pili naomba leo nikupitishe katika maswali mengine kuhusu nchi unayoishi;
SWALI LA TATU:
( 3 ) Malango ya nchi yenu yanapitisha na kuingiza vitu gani katika nchi?.
Nahumu 3:13 Maombolezo 4:12 Nehemia 13:19
Nataka nikuulize katika malango ya nchi yenu yanapitisha na kuingiza vitu gani katika nchi na maisha ya wananchi? Malango mengi ya nchi ukiyafuatilia rohoni yanaingiza vitu vibaya sana kwaajili ya nchi na vitu hivyo vimeyafunga maisha ya wananchi wanaoishi katika nchi, na kanisa limelala haliombei malango ya nchi na hivyo maadui hupitisha vitu vyao vya uovu katika nchi, nakuomba wewe kanisa amka na uhakikishe kwamba kila siku unayaombea malango ya nchi yenu mbele za Mungu.
Hakikisheni mnayakabidhi malango ya nchi yenu kwa Mungu ili Shetani na maadui wasiweze kuyatumia na kuifunga nchi na maisha yenu wananchi.
SWALI LA NNE:
( 4 ) Je nchi yenu niya nani kiroho?.
2Samwel 3:12 Zaburi 33:12 2Waflme 17:24-276
Nchi unayoishi niya nani kiroho? Najua hujawahi kujiuliza na kutafakari hili swali na matokeoa yake unaishi katika nchi usiyojua niya nani kiroho na matokeo yake mwenye nchi yenu rohoni amekuwa anayaongoza maisha yako hata kama hutaki. Unapofuatilia kwenye ulimwengu wa roho nchi nyingi niza miungu migeni sio nchi za Mungu katika Yesu Kristo na kuishi katika nchi ambayo niya miungu utambue wazi kwamba hiyo miungu ndio itakayohusika na nchi na maisha ya wananchi waliomo ndani yake.
Tafakari sana hili swali je nchi yenu niya nani kiroho? Swala sio kuzaliwa katika nchi au kuwa na kitambulisho cha uraia nataka ujue kwamba katika ulimwengu wa roho nchi inaweza kuwa ya Mungu au miungu, hivyo hakikisha kwamba mnaingia kwenye maombi na kuiombea sana nchi yenu na kuitoa kwenye mikono ya shetani/miungu na kisha kuingiza nchi kwenye mikono ya Mungu ili Mungu aweze kuisimamia nchi yenu na maisha yenu wananchi ya kila siku.
SWALI LA TANO:
( 5 ) Je kiti cha Urais katika nchi yenu kimebeba vitu gani kwaajili ya nchi?.
2Samwel 21:1 Waebrania 4:16
Kiti cha urais katika nchi kimebeba vitu mbalimbali vya kiroho nataka nikuulize katika nchi unayoishi kile kiti cha urais wenu kimebeba vitu gani kwaajili ya nchi na maisha yenu? Nataka ujue kwamba kuna tofauti ya Rais na kiti cha Urais kwasababu rais akimaliza muda wake wa uongozi huondoka ila kiti cha urais bado kinabakia katika nchi yenu.
Ni watu wangapi ambao mnaoishi katika nchi mnatambua kiti chenu cha urais kimebeba vitu gani? Unapofuatilia matatizo mengi katika nchi na maisha ya wananchi yanayowatesa toka kizazi hadi kizazi yako yanayotokea katika kiti cha urais cha nchi yao. Kanisa halina utaratibu wa kuombea kiti cha urais mbele za Mungu na matokeo yake nchi kupitia nyakati ngumu nakuomba uwe unakiombea sana kiti cha urais katika nchi yenu na kupangua vitu vyote visivyofaa vilivyobebwa katika kiti cha urais wenu na kukabidhi hicho kiti cha urais chini ya utawala wa Mungu.
Mnaweza kuwa na rais mzuri mwenye maono makubwa sana kwaajili ya nchi yenu na maisha yenu lakini kiroho akakwamishwa na vitu vilivyopo kwenye kiti cha urais anachokitumia kutawala ndio maana nasisitiza kwamba hakikisheni mnakiombea sana kiti cha urais katika nchi yenu.
✔️ Kwa siku ya leo naomba utafakari maswali haya kuhusu nchi yenu na kuomba mbele za Mungu, tukutane siku ya kesho ambapo bado tutaendelea na eneo hili la nchi. Nisaidie kuwashirikisha wengine masomo haya na kwenye magroup mengine uliyopo.
Kwa mawasiliano nami utanipata kwa namba hizi:
Vodacom M-PESA+255 765 867574 ( WhatsApp ).
Airtel Money +255 785 855785.
Tigo Money +255 673 784197.
Kwa Email address ni Pastorkibiriti@gmail.com
Mimi ni Mwalimu wa Neno la Mungu la Maarifa
Samwel Kibiriti.
Mei 21, 2021
Mbeya Tanzania.
@Kibiriti2021
Karibu katika semina ya siku ya kesho ambapo tutaendelea kupokea maarifa ya Neno la Mungu.
No comments:
Post a Comment