Post Top Ad

Post Top Ad

Saturday, February 4, 2017

AINA TOFAUTI ZA MAOMBI

AINA TOFAUTI ZA MAOMBI.
 
Bwana Yesu asifiwe rafiki yangu katika Kristo Yesu, nakukaribisha tena siku hii ya leo ndani ya darasa la chuo hiki cha kupokea maarifa ya kiroho.
 
{ KIPENGELE CHA NNE }.
 
 Nataka tena siku ya leo tuangalie aina nyingine ya maombi ambayo unatakiwa kumuomba Mungu.
 
 
KUNA MAOMBI YA KINADHIRI.
 
Hii ni aina nyingine ya Maombi ambayo unatakiwa kumuomba Mungu na ukimwendea Mungu kwa mfumo wa maombi haya ya kinadhiri atakusikia na kutenda kwako sawa sawa na ulivyomuomba.
 
Maombi ya kinadhiri ni maombi ya jinsi gani?
 
Maombi ya kinadhiri ni maombi unayomuomba Mungu  kwamba akutendee jambo au akuvushe mahali hapo pagumu unapopitia kwenye maisha yako ambapo huoni msaada wowowte wa kutoka na unamuahidi Mungu kwamba ukinivusha hapa au ukinitendea hiki, mimi nitafanya kwako jambo fulani.
 
unapoenda mbele za Mungu kwa jinsi hiyo wewe kumuomba akuvushe mahali pagumu halafu akifanya hivyo na wewe utamtolea kitu fulani, nakuambia hivi Mungu Baba atakutendea kwa haraka sana hicho ulichomuomba kwa sababu anafahamu kwamba akikutendea wewe nawe kuna jambo utakalolifanya kwaajili yake Mungu.
 
ngoja nikupitishe kwenye mifano miwili tu ya watu ambao walienda mbele za Mungu kwa njia hii ya maombi ya kinadhiri na Mungu aliwajibu
 
{ 1 } Hana.
 
Hana alikuwa ni mke wa Elkana, na huyu mwanamke waliolewa wawili mwenzake alikuwa anaitwa Penina. Sasa huyu Hana alikuwa hana watoto lakini mwenzake alikuwa na watoto na kila siku Penina alikuwa anamdhihaki na kumsema vibaya Hana kwa sababu alikuwa ni tasa.
 
Biblia inasema siku moja baada ya Hana kumaliza kutoa sadaka huko Shilo akainuka na kukimbilia hekaluni kwa Mungu ambapo kuhani alikuwa ni mzee Eli, sasa angalia Hana alivyomuomba Mungu
 
1SAMWEL 1
10 Naye huyo mwanamke alikuwa na uchungu rohoni mwake, akamwomba BWANA, akalia sana.
 
11 Akaweka nadhiri, akasema, Ee BWANA wa majeshi, ikiwa wewe utaliangalia teso la mjakazi wako, na kunikumbuka, wala usinisahau mimi mjakazi wako, na kunipa mimi mjakazi wako mtoto mume, ndipo mimi nitakapompa BWANA huyo mtoto siku zote za maisha yake, wala wembe hautamfikilia kichwani kamwe.
 
12 Ikawa, hapo alipodumu kuomba mbele za BWANA, Eli akamwangalia kinywa chake.
 
17 Ndipo Eli akajibu, akasema, Enenda kwa amani, na Mungu wa Israeli akujalie haja yako uliyomwomba.
 
unamuona huyu mwanamke Hana anamwendea Mungu kwa mfumo huu wa maombi ya kinadhiri na anaweka nadhiri yake ya midomo kwa Mungu kwamba ampatie mtoto wa kiume na akamwambia Mungu kwamba akimpatia mtoto huyo atamtoa kwa Mungu na atakuwa mtumishi wa kutumika kwenye madhabahu yake maisha yake yote.
 
Sasa angalia alivyomuomba Mungu kwa maombi haya ya kinadhiri Mungu alifanya nini? je alimjibu maombi yake au hakumjibu?
 
1SAMWEL 1
 
20 Ikawa, wakati ulipowadia, Hana akachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; akamwita jina lake Samweli, akasema, Kwa kuwa nimemwomba kwa BWANA.
 
  Unamuona Mungu anayajibu maombi haya ya Hana ya kinadhiri aliyomuomba na kumpatia mtoto wa kiume sawa sawa na alivyomuomba Mungu.
 
Na baada ya Mungu kuyajibu maombi hayo ya Hana na kumtimizia alichomuomba unaona Hana naye anaitimiza ile nadhiri aliyomwekea Mungu "Naliomba nipewe mtoto huyu; BWANA akanipa dua yangu niliyomwomba; kwa sababu hiyo mimi nimempa BWANA mtoto huyu; wakati wote atakaokuwa hai amepewa BWANA. Naye akamwabudu BWANA huko" { mstari wa 27 na 28 }.
 
Sijajua na wewe unapolisoma somo hili uko katika hali gani ya kimaisha, Hana hakuwa na watoto na mke mwenzake alimdharau na kumbeza sana kila siku ikabidi aingie kwenye mfumo huu wa maombi ya kinadhiri, je wewe unasongwa na mambo gani kwenye maisha yako? usikate tamaa hebu mwendee Mungu kwa maombi kama haya ya kinadhiri na utaona jambo ambalo Mungu Baba atakutendea kwenye maisha yako.
 
{ 2 } Yakobo. 
 
Huyu ndugu Yakobo naye alimwendea Mungu kwa maombi haya ya kinadhiri ni kipindi ambacho alimkimbia kaka yake Esau ambaye alikuwa anamwinda ili amuue baada ya kuchukua mbaraka wake kutoka kwa baba yao Isack, ndipo mama yake Rebeka akamwambia Yakobo akimbie aende kwa mjomba wake Labani ili ajifiche huko kwanza ampaka zitulie hasira ya kaka yake.
 
Yakobo alipokimbia alikuwa hana kitu chochote kile na hata kule alikokua anaenda alikuwa hakufahamu, kwa ujumla alikuwa hana kabisa mwelekeo wa maisha hajui ataishije, atavaa nini, atakula nini n.k ndipo akamwendea Mungu aliye hai kwa maombi haya ya kinadhiri, angalia mistari hii,
 
MWANZO 28
 
20 Yakobo akaweka nadhiri akisema, Mungu akiwa pamoja nami, akinilinda katika njia niiendeayo, na kunipa chakula nile, na nguo nivae;
 
21 Nami nikirudi kwa amani nyumbani kwa baba yangu, ndipo BWANA atakuwa Mungu wangu.
 
22 Na jiwe hili nililolisimamisha kama nguzo litakuwa nyumba ya Mungu; na katika kila atakalonipa hakika nitakutolea wewe sehemu ya kumi.
 
Unayaona mazingira ya kimaisha aliyokuwa nayo Yakobo yalikuwa ni mabaya sana kwani alikuwa hana chakula cha kula, hana nguo, na matatizo mbalimbali akamwendea Mungu kwa maombi haya ya kinadhiri na Mungu akamjibu na kumtendea makuu mpaka alipokuwa anatoka nyumbani kwa huyo mjomba wake Labani huyu Yakobo alikuwa ni tajiri.
 
Sijajua na wewe mama yangu, baba yangu, kaka yangu, dada yangu, mdogo wangu na mtoto uko kwenye hali gani ya kimaisha inawezekana na wewe ni kama Yakobo huna chochote na hujui kabisa mwelekeo wa maisha yako utakuwaje umekata tamaa, nakuomba nenda mbele za Mungu kwa maombi kama haya ya kinadhiri.
 
Mweleze kabisa Mungu hali yako uliyonayo ya kimaisha usimfiche na mwambie kabisa kwamba Mungu nimefika mwisho nakuja kwako kwa maombi haya ya kinadhiri naweka nadhiri kwako kwamba ukinivusha kwenye haya maisha, matatizo, madeni, shida n.k mimi nitakutolea hiki/ nitakupatia hiki kama sadaka yangu ya nadhiri hii. ukishamuomba Mungu Baba hivyo utashangaa haraka sana anakujibu hayo maombi yako, ila kumbuka Mungu akishakutendea ni lazima na wewe ufanye ulichomwahidi kwa kukitoa sawa?
 
Naamini kwamba utafanyia kazi somo hili na utamwendea Mungu kwa mfumo wa maombi haya ya kinadhiri, Roho Mtakatifu akusaidie kuliingiza kwenye matendo ili uone baraka zake toka kwa Mungu.
 
Tukutane tena siku ya kesho ndani ya darsa hili la chuo hiki, wakaribishe na wengine.
Mkono wa Mungu Baba ukupiganie na kukushindia katika maisha yako.

KAULI MBIU MWAKA 2017.
  
{ 1 }  Acha dhambi
 
       { 2 } Yesu Kristo anakuja.
 
                                  { 3 } Ishi katika maisha ya utakatifu kila siku.
 
 Mimi ni mwalimu Samwel Kibiriti rafiki yako katika Kristo Yesu.
 
@Kibiriti 2017, February 4.

No comments:

Post a Comment

Featured Post

JINSI MISINGI YA VIZAZI INAVYOWEZA KUKAMATA MAISHA YAKO.

Fahamu kwamba misingi ni chanzo au asili au chimbuko la mtu. Na msingi wako wa vizazi unatokana na ukoo wako na kabila lako.      ...