AINA TOFAUTI ZA MAOMBI.
Shalom Rafiki yangu katika Kristo Yesu nakukaribisha tena siku hii ya Leo katika darasa letu hili la kupokea maarifa na kanuni hizi za kiroho.
{ KIPENGELE CHA TATU. }
KUNA MAOMBI YA KWENDA MBELE ZA MUNGU KWA KULIA.
➡ Unatakiwa uende mbele za Mungu kwa kulia, maombi haya ya kulia ni maombi ya pekee na yana mguso wa aina yake mbele za Mungu.
✔ Maombi haya ya kulia huingia kwenye moyo wa Mungu kwa kina na huleta majibu ya haraka kwa huyu anayeyaomba. Ni njia yenye majibu ya haraka.
➡ Kwenda mbele za Mungu kwa Maombi ya kulia huonyesha Unyenyekevu na moyo uliopondeka mbele za Mungu, na kwamba huna tegemeo jingine yeye asipotokea na kukujibu.
✔ Kuna mazingira ambayo mwanadamu anaweza kufika ambapo akiangalia kila kitu haoni msaada wowote na hajui atatokaje katika mazingira kama hayo, saa nyingine unakuta kila mtu amekaa mbali nae hata marafiki na ndugu wamemuacha hajui afanye nini, unachotakiwa ni kwenda mbele za Mungu kwa Maombi haya ya kulia, unamlilia Mungu na kumweleza kabisa kwamba Mungu ukinyamaza hapa Mimi naangamia, nakwambia Mungu hawezi kunyamaza na kuyaacha hayo machozi yako yaende bure Bali ataingilia kati maisha yako na kukutoa kwenye hayo mazingira magumu.
YEREMIA 31
"9 Watakuja kwa kulia, na kwa Maombi nitawaongoza; nitawaendesha penye mito ya maji, katika njia iliyonyoka; katika njia hiyo hawatajikwaa; maana Mimi ni baba wa Israeli, na Efraimu ni mzaliwa wa kwanza wangu".
Bwana anasema watakuja kwa kulia na kwa Maombi nitawaongoza, katika njia iliyonyooka, ambayo hawatajikwaa yaani hawatapata hasara.
➡ Kwa hiyo hii ina maanisha nini? Pale ambapo huoni njia iliyonyooka kwenye maisha yako na hujui ataendaje mbele yako unachotakiwa nenda mbele za Mungu kwa Maombi haya ya kulia, naye anasema atakuongoza katika njia iliyonyooka.
Tujifunze kwa Hezekia alipokuwa ameumwa kiasi cha kufa alilia sana sana mbele za Mungu na Mungu akamjibu pale pale.
ISAYA 38
1 Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, BWANA asema hivi; Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona".
2 Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba BWANA",
3 akasema, Ee BWANA, kumbuka haya, nakusihi, kwamba nimekwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana"
4 Ikawa, neno la BWANA likamjia Isaya, kusema"
5 Enenda ukamwambie Hezekia, BWANA, Mungu wa Daudi, baba yako, asema hivi, Mimi nimeyasikia Maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitaziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano".
Huyu Hezekia alitakiwa afe na Nabii alishafika kuthibitisha kifo chake, lakini Hezekia kwa kwenda kwake mbele za Mungu kwa kulia, hukumu iligeuzwa pale pale na tamko jipya likatolewa la miaka yake kuongezwa zaidi.
BWANA akamwambia Nabii Isaya nimesikia maombi yake, na nimeyaona Machozi yake, nitaongeza miaka yake. Machozi ni jibu la haraka toka kwa Mungu kwa ajili ya muhitaji wake.
✔ Hezekia alilia sana sana maana alikuwa hana namna nyingine ya kuishi, isipokuwa jibu la Mungu tu pekee.
Wako watu wanaofikili mtu anayemwendea BWANA kwa maombi ya kulia hana Imani huo ni utoto mchanga kiroho kuamini hivyo, maombi ya kulia mbele za Mungu yapo na Biblia imelieleza jambo hili kama nilivyokuonyesha hiyo mistari michache hapo juu.
➡ Ukienda mbele za Mungu kwa Maombi ya kulia ni lazima atajifunua kwako na jibu la haja yako utalipata. Jitoe kwa Mungu katika maombi haya nawe utaona ushindi katika kila eneo la maisha yako.
➡ Sifahamu muda huu unaposoma somo hili uko katika hali gani kimaisha? Inawezekana umebakia kama Hezekia huna namna ya kuishi magonjwa yanataka kukuua, madeni yamekuandama, hujui utawalisha nini watoto wako, biashara ni hasara tu, kazini wanatishia kukufukuza, kodi ya nyumba huna na kwenye nyumba anataka kukufukuza, unafeli sana kwenye masomo, Ndoa yako inataka kuvunyika n.k
Na wewe hujui ufanye nini umekata tamaa ya kuishi unaona kama vile Mungu amekutenga na kukuacha, naomba sikia Neno hilo tumaini lipo na Mungu Baba hajakusahau, hebu ingia kwenye maombi nenda mbele za Mungu kwa Maombi haya ya kulia mwambie Mungu aina msaada popote pale nimekata tamaa ya kuishi kutokana na haya yanayoniandama, lia sana mbele za Mungu na Mungu aliyemtokezea Hezekia atakutokezea na wewe na atayaona machozi yako naye atakuondoa katika hiyo shida na dhiki na mateso yako, naye atakuongoza katika njia iliyonyooka sawa sawa na mapenzi yake.
Kwa Leo naishia hapa tukutane tena siku ya kesho
nitakapokuonyesha aina nyingine ya maombi. Fanyia kazi hili.
Kwa mawasiliano nami utanipata kwa simu
Voda 0765 867574
Tigo 0673 784197
Airtel 0785 855785
Mimi ni Mwalimu Samwel Kibiriti Rafiki yako atika Kristo Yesu
Neema ya Kristo Yesu iwe pamoja nanyi wote.
@kibiriti 2017, 3 February.
AMINA ubarikiwe sana
ReplyDelete