Post Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, June 16, 2021

 Semina ya siku 30 ( Christ For All People Church- Mbeya ).

KUYASHUGHULIKIA MALANGO YA KIROHO YANAYOGUSA MFUMO WAKO WA MAISHA YA KILA SIKU.

         Day 10 ya semina.

Senior Pastor Samwel Kibiriti.

Bwana Yesu Kristo atukuzwe mwana wa Mungu karibu tuendelee na semina ya siku ya leo.

KUSHUGHULIKIA LANGO LA NAFSI YAKO ( A ).

Zaburi 25:20 Kutoka 32:7 Kumbukumbu 4:16 Hesabu 11:18 Zaburi 7:5  Hesabu 31:50

Baada ya kumaliza kukufundisha kuhusu kupambana na lango la nchi unayoishi na kujifungua kwenye madhabahu za nchi zilizofunga maisha yako, leo nataka tuanze somo hili la lango la Nafsi yako ambapo tutajifunza kwa siku 3 kuhusua lango hili, na Mungu atasema nawe na kuifungua nafsi yako. Wako aatu wengi sana hawajui jinsi nafsi zao zinazofanya kazi kiroho na pia lango hili la nafsi kwa watu wengi limeshikiliwa na nguvu za giza ndio maana nafsi zao zinateseka na kutumikishwa sana kila siku wakiwa katika usingizi na kwenye ndoto bila kupata msaada wa kuwaweka huru.


SABABU YA VITA KATIKA NAFSI YAKO.

Naomba leo nikueleze sababu za vita katika nafsi yako na katika nafsi za watoto wako na wazazi wako na ndugu zako. Kuna vita kubwa sana iliyoelekezwa kwenye nafsi za wanadamu na hii vita imesababisha nafsi nyingi kutokufanya kazi kama vile zilivyoumbwa na Mungu kwenye maisha ya watu. Na wengi hawajui kwanini wanakutana na vita sana kila siku katika nafsi zao, mimi kama mwalimu wa Neno la Mungu la Maarifa naomba nikueleze hizo sababu kibiblia zinazosababisha uko kwenye vita ya nafsi yako kila siku.


                SABABU YA KWANZA:

( 1 ) Nafsi ndio inayoweza kutafsiri Sauti ya roho na sauti ya mwili wako ili vielewane

Wagalatia 5:16-25

🔵 Mungu aliumba roho na nafasi na mwili wako na katika utendaji kazi wa maeneo haya 3 ni kwamba ndani ya roho yako kuna sauti na katika mwili wako kuna sauti hivyo biblia inasema kwamba roho na mwili hazielewani na nafsi yako ndio iliyobebeshwa jukumu na Mungu kutafsiri sauti ya roho na mwili vielewane ili uweze kuyafanya mapenzi ya Mungu katika maisha yako. Nafsi yako inapofungwa kiroho itashindwa kutafsiri sauti ya roho na mwili na hivyo kushindwa kuelewana na kujikuta huishi maisha ya kuyafanya na kuyatimiza mapenzi ya Mungu hapa duniani kila siku.

❌Je nafsi yako inatafsiri sawasawa sauti ya roho na mwili wako na kuelewana katika kuyafanya mapenzi ya Mungu? Hakikisha unafanya maombi ya kuifungua nafsi yako mahali ilipofungwa ili iweze kuwa huru na wewe uweze kuyafanya mapenzi ya Mungu kwenye maisha yako, pia omba Mungu aurejeshe ule uweza wake katika nafsi yako.


                SABABU YA PILI:

( 2 ) Nafsi ndio iliyobeba Maisha yako unayoishi hapa duniani

Ayubu 10:1

Maisha yako unayoishi leo hii yawe mazuri au mabaya chanzo ni nafsi yako wala sio roho yako wala mwili wako kwasababu Mungu alipoiumba nafsi yako ndio aliyoibebesha jukumu la kuongoza maisha yako hapa duniani.  Kwahiyo kwa lugha rahisi tunasema kwamba unavyoishi leo ni matokeo ya nafsi yako ilivyo na inavyofanya kazi rohoni. Huwezi kuwa na maisha unayoyatamani kama nafsi yako imefungwa utakuwa unayasimulia tu hayo maisha pasipo kuyaishi kwa uhalisia hapa duniani hivyo ni jambo la msingi kujua kwamba nafsi yako iko huru au imefungwa ili uweze kuiombea mbele za Mungu.

❌Je maisha unayoyaishi sasa ndivyo Mungu alivyokupangia uwe nayo? Jibu ni hapana kuna maisha mazuri sana wakati Mungu alipokuumba alikuandalia na kukupangia ila kwasababu nafsi yako imefungwa umejikuta huyaishi hayo maisha. Hakikisha unapata msaada wa kiroho kufunguliwa kwa nafsi yako ili uweze kurudi katika maisha yako halisi uliyokusudiwa na Mungu, na muombe Mungu ayarejeshe maisha yako halisi ili uweze kuyaishi hapa duniani kwa kipindi atakachokuweka kuishi.


                       SABABU YA TATU:

( 3 ) Nafsi ndio iliyobeba kiu ya wewe kumtafuta Mungu kwenye maisha yako

Zaburi 42:2 Yohana 7:37 Zaburi 143:6 Yeremia 29:13

Wakristo wengi ndani yao hawana kiu kabisa ya kumtafuta Mungu na kuutafuta uso wa Mungu kwasababu ile kiu imeshaondolewa ndani ya nafsi zao ndio maana unawakuta ni wakristo wa mazoea tu makanisani. Nataka ufahamu kwamba Mungu aliweka kitu kinachoitwa kiu/shauku ndani ya nafsi na kiu hiyo aliyoiweka sio ya kutafuta kufanya kitu chochote kile hapana ameiweka hiyo kiu ili moyo wako umtafute sana Mungu kila siku ya maisha, kwasababu mwenye kuyajua maisha yako ni Mungu pekee wala sio mwanadamu wala kiumbe yoyote yule hivyo unapoweka jitihada kubwa ya kumtafuta Mungu aliahidi kwamba ataonekana kwako.

❌Je ndani ya nafsi yako kuna kiu ya kumtafuta Mungu kila siku? Hakikisha unaingia katika maombi na kuifungua nafsi yako na kumuomba Mungu akurejeshee kiu yake ya wewe kumtafuta yeye zaidi ya unavyotafuta pesa kwani ukimpata Mungu umepata kila kitu katika maisha yako.


                        SABABU YA NNE:

( 4 ) Nafsi ndio iliyobeba Mafanikio ya maisha yako

Zaburi 25:13  3Yohana 1:2

Mafanikio ya maisha yako hayako kwenye roho yako wala hayapo kwenye mwili wako au kwenye utendaji kazi wako sana hapa duniani bali mafanikio yako yamebebwa ndani ya nafsi, kwahiyo nafsi yako ndio inayokuamulia viwango vya kufanikiwa kimaisha hapa duniani. Mtu yoyote ambaye nafsi yake imefungwa hawezi kufanikiwa kimaisha hata kama atajitahidi vipi kufanya kazi hili wengi hawalifahamu. 

❌Mafanikio ya maisha yako yamewekwa na Mungu katika nafsi yako hivyo hakikisha unaombea sana nafsi yako na kuifungua ili uweze kuishi maisha ya mafanikio hapa duniani sawasawa na kusudi la Mungu la kukuumba.


                    SABABU YA TANO:

( 5 ) Nafsi ndio Injini ya kufanya kazi kwa mtu hapa duniani

Mithali 16:26  Zaburi 104:23  Mhubiri 3:13

Injini ya mwanadamu ya kufanya kazi za mikono sio mwili bali ni nafsi yake  na wengi hawafahamu hili ndio maana watu wengi unawakuta wanafanya kazi za mikono kwa kutumia miili yao wakati huo nafsi zao zimefungwa rohoni na kujikuta wanajitahidi kweli kufanya kazi lakini maisha yao hayabadiliki kabisa kila siku. Nafsi yako ndio injini ya kufanya kazi ili kufanikiwa kwenye kazi zako kwahiyo injini inapofungwa hakuna kitu kitasogea kwako. 

Nafsi ndio inayotakiwa ishirikiane na mwili kufanya kazi za mikono kwa pamoja lakini sivyo ilivyo wengi sana mwili ndio unaofanya kazi bila kushirikiana na nafsi ndio maana hawafanikiwi wala kupata matokeo yale waliyokusudiwa kuyapata kupitia kazi zao za mikono. Kufanya kazi kubwa kwa mwili wako huku nafsi yako ikiwa imechukuliwa mateka kiroho ni kujichosha bure bila faida yoyote katika maisha yako ndio leo unakutana na watu wengi wanaolalamika kuteseka na kuchoka kupitia kazi wanazozifanya bila kufanikiwa na kustawi wao wakidhania tatizo ni kazi kumbe tatizo lipo kiroho nafsi zao zimeshafungwa na kuibiwa na kutekwa na maadui.

❌Je nafsi yako inafanya kazi kwa kushirikiana na mwili wako kwa ukamilifu au unatumia mwili peke yake kufanya kazi huku nafsi yako ikiwa kifungoni? Ingia kwenye maombi ya nguvu ya kuifungua nafsi yako katika utendaji kazi wake wa kila siku kwenye maisha yako.


               SABABU YA SITA:

( 6 ) Nafsi ndio iliyobeba Akili na mawazo na fikira

Akili na mawazo na fikira Mungu aliziweka ndani ya nafsi kwahiyo nafsi yako ikibanwa na shetani rohoni ujue akili zako na mawazo yako na fikira zako nazo pia zitakuwa zimebanwa, pia nafsi yako ikitekwa nyara rohoni ujue pia na akili zako zimetekwa na mawazo yako yametekwa na fikira zako  zitakuwa zimetekwa na hivyo kushindwa kutumika sawasawa kama Mungu alivyoviumba na kuziweka ndani yako kwaajili ya maisha yako hapa duniani.

 Aliyeshikilia nafsi yako kwenye ulimwengu wa kiroho ndiye huyo atakayeibana nafsi yako na kuiongoza vyovyote atakavyo yeye na kujikuta huwezi kufanya yale unayotakiwa kuyafanya bali unafanya vitu ambavyo hata wewe na wanaokuzunguka wanashangaa tu kwasababu nafsi yako inaongozwa vibaya tofauti na mapenzi ya Mungu.

🔶 Nimeweza kukuonyesha sababu za kiroho kwanini nafsi yako inakutana na vita ni kwasababu ya vitu ilivyovibeba kwaajili ya maisha yako ya kila siku hapa duniani, hivyo ingia katika maombi na kuiombea kwa nguvu nafsi yako hadi ifunguliwe na kuhuishwa na Mungu. Hii vita ya nafsi yako kama hutapata msaada mkubwa wa kiroho utajikuta na maisha ya kuteseka na kuhangaika tu hapa duniani na hilo sio mpango wa Mungu aliyekuumba na kukuleta hapa duniani. Matatizo makubwa ya maisha ya watu waliyonayo yako kwenye nafsi zao kwasababu haziko sawasawa kiroho kabisa kwenye utendajo kazi.


✔️ Kwa leo semina yetu inaishia hapa tukutane siku ya kesho ambapo nitasema nawe kuhusiana na eneo la akili katika nafsi yako. Nakuomba unisaidie kuwashirikisha watu wengine masomo haya ili wapokee maarifa ya kuwatoa katika mateso wanayopitia kimaisha.

Kwa mawasiliano nami utanipata kwa namba hizi:

Vodacom +255 765 867574 ( WhatsApp ).

Airtel +255 785 855785

Tigo +255 673 784197

Kwa Email address ni Pastorkibiriti@gmail.com



Mimi ni Mwalimu wa Neno la Mungu la Maarifa

          Samwel Kibiriti.

Mei 24, 2021

@Kibiriti2021

Kumbuka Bwana Yesu anarudi hakikisha kwamba umeokoka na kuishi maisha ya utakatifu huku ukiyafanya mapenzi ya Mungu kwenye maisha yako.

No comments:

Post a Comment

Featured Post

JINSI MISINGI YA VIZAZI INAVYOWEZA KUKAMATA MAISHA YAKO.

Fahamu kwamba misingi ni chanzo au asili au chimbuko la mtu. Na msingi wako wa vizazi unatokana na ukoo wako na kabila lako.      ...