Post Top Ad

Post Top Ad

Saturday, May 29, 2021

 Semina ya Siku 30 ( Christ For All People Church- Mbeya ).

KUYASHUGHULIKIA MALANGO YA KIROHO YANAYOGUSA MFUMO WAKO WA MAISHA YA KILA SIKU.

             Day 2 ya Semina.

Na Mwalimu Samwel Kibiriti.

Bwana Yesu Kristo asifiwe mwana wa Mungu karibu siku ya leo ya semina na Mungu atasema nawe na kukuhudumia, leo tujifunze jambo hili;

MFUMO WAKO WA MAISHA YA KILA SIKU UNAGUSWA NA MAMBO YAFUATAYO ( A ):

Mwanzo 1:26-27  1Thesalonike 5:23

🔵 Siku ya leo nataka tujifunze eneo hili la mfumo wako wa maisha. Kama nilivyosema jana kwamba maisha ya mwanadamu yamejengwa katika mfumo wa kuzaliwa na kufa na ndani ya mfumo wa maisha kuna kusoma shule, kuoa&kuolewa, kufanya kazi, kuwa na furaha au kukosa furaha, kulia na kucheka n.k hivyo nataka nikuonyeshe maeneo ambayo yanagusa mfumo wako wa maisha ya kila siku. 

Haya maeneo hakikisha kwamba unayaombea sana kwa maombi yako kwasababu uwe unajua au haujui haya maeneo yanagusa mfumo wako wa maisha ya kila siku inategemea maisha yako yanaguswa kwa namna mzuri au namna isiyokuwa nzuri inategemea na kile kinachoendelea katika maeneo haya kila siku ndio maana nikakuambia omba sana mbele za Mungu kwaajili ya maeneo haya yanayogusa mfumo wako wa maisha ya kila siku.

( 1 ) Mfumo wangu wa Maisha unaguswa na Malango ya kiroho.

Kumbukumbu la torati 28:52 Maombolezo 4:12

🔶 Malango ya kiroho yanagusa mfumo wako wa maisha ya kila unayoyaishi hapa duniani na kuna watu wengi sana maisha yao hayaendelei mbele na hawafanikiwi na kufikia malengo yao kwasababu wamefungwa na kubanwa kiroho kwenye malango ya kiroho. Wakristo wengi hawaombeagi malango yao ya kiroho hivyo kukuta maadui wamepita hapo na kuyafunga maisha yao.

❌ Je wewe malango yako ya kiroho yanafanyaje kazi kuhusiana na maisha yako? Je malango ya familia unayoishi na nchi unayoishi na mji unaoishi yanafanyaje kazi kila siku kuhusiana na maisha yenu?

Hakikisha kwamba unayaombea sana malango ya kiroho yanayogusa maisha yako ya kila siku, lakini kumbuka kabla hujaombea malango ya kiroho ni lazima ujiweke wakfu kwa Mungu kama nilivyokufundisha katika semina ya jana.

✔️ Kwa maarifa makubwa zaidi kuhusu malango ya kiroho karibu ujipatie nakala ya kitabu changu nilichoandika kiitwacho  MAOMBI YA KUWEKA WAKFU KWA MUNGU MALANGO YA KIROHO YANAYOGUSA MAISHA YAKO, ndani ya kitabu nimefundisha mambo mengi sana yatakayokuwa msaada kwako kitabu ni Tsh 8,000 ( Elfu nane ) wasiliana nami kwa maelezo zaidi.

( 2 ) Mfumo wangu wa maisha unaguswa na Mbingu za kiroho.

Kumbukumbu la torati 28:23  Mathayo 3:16-17

🔶 Mbingu za kiroho zinahusika kwa asilimia kubwa sana kila siku kugusa mfumo wako wa maisha unayoishi hapa duniani na kuna mambo mengi sana ambayo yanafanyika kwenye mbingu zako za kiroho na mambo hayo yamesababisha maisha yako kufungwa na kujikuta unaishi kwa mateso hapa duniani. Kuna watu maisha yao yamefungwa kwenye mbingu zao za kiroho na kuna familia na miji na nchi maisha ya watu waliomo ndani yake yamefungwa kwenye mbingu zao za kiroho.

❌ Je wewe mbingu zako za kiroho zinafanyaje kazi kila siku? Ni vitu gani vinavyoendelea kwenye mbingu zako za kiroho? Nataka utambue kwamba chochote kinachoendelea katika mbingu zako za kiroho lazima kitaonekana katika maisha yako hapa duniani.

Hakikisha unaziombea sana mbingu zako za kiroho kila siku na kuyafungua maisha yako yaliyofungwa kwenye mbingu za kiroho pia yafungue maisha ya watoto wako na ndugu zako.

( 3 ) Mfumo wangu wa maisha unaguswa na Anga la kiroho mahali nilipo.

Ezekieli 10:1  Danieli 10:1,13,20

🔶 Anga la kiroho linahusika sana kila siku kugusa mfumo wako wa maisha ya kila siku unayoyaishi hapa duniani, hivyo unatakiwa sana kuliombea anga la kiroho mahali unapoishi kwasababu shetani na miungu wakifanikiwa kulishika anga lako la kiroho mahali unapoishi kuna vitu vingi sana watavifanya ikiwepo kuzuia majibu yako ya maombi na kusababisha mambo kutokwenda sawasawa kwenye maisha yako kama ulivyokusudiwa na Mungu.

❌ Je anga la kiroho mahali unapoishi limeshikiliwa na nani kiroho? Hakikisha kwamba unafanya sana maombi ya kulifungua anga la kiroho na kupambana na roho zote zinazotenda kazi kwenye anga la kiroho mahali unapoishi na kufanya kazi.

( 4 ) Mfumo wangu wa maisha unaguswa na utendaji kazi wa Ardhi.

Mwanzo 4:10-12  Yeremia 22:29-30

🔶 Utendaji kazi ulioko ndani ya ardhi unayoikanyaga na kuishi unahusika sana katika mfumo wako wa maisha ya kila siku, kuna watu maisha yao yamefungwa kwenye ardhi lakini wengine wanakutana na vita mbalimbali ambazo chanzo chake ni ardhi pia wako wengine wametengenezewa na ardhi maisha ya kutangatanga na kutokuwa na kikao na kutofanikiwa katika yale wanayoyatenda kwenye maisha yao.

❌ Je ardhi unayoikanyaga kila siku na ardhi mahali unapoishi inafanyaje kazi kuhusu maisha yako ya kila siku? Hakikisha kwamba unaingia katika maombi na kuiombea ardhi kwenye utendaji kazi wake na kuyafungua maisha yako yaliyofungwa katika ardhi.

( 5 ) Mfumo wangu wa maisha unaguswa na matumizi ya Muda.

Mhubiri 3:1  Waefeso 5:15-17

🔶 Matumizi yako ya muda wa masaa 24 ya siku unahusika sana katika kugusa mfumo wako wa maisha na watu wengi wamekuwa na maisha mabaya kwasababu wanautumia muda kiujinga hawatumii muda kwa hekima. Kitendo cha kupoteza muda kinaharibu maisha yako hakikisha kwamba unatumia vizuri sana muda wako wa kila siku kwasababu maisha ya mwanadamu yamejengwa katika muda na kusudi la kuumbwa kwako limeunganishwa na muda hivyo kuwa na adhabu na nidhamu katika matumizi ya muda wako kila siku.

❌Je wewe unatumiaje muda wa kila siku wa masaa 24? Unatumia muda kwa hekima au unatumia muda kwa ujinga? Hakikisha unamuomba Mungu akujalie hekima yake ya wewe kuutumia muda sawasawa na mapenzi yake ili maisha yako yawe mazuri hapa duniani na uweze kulitumikia vyema kusudi lako la kuumbwa na Mungu.

( 6 ) Mfumo wangu wa maisha unaguswa na Ndoto ninazoziota nikilaa.

Ayubu 4:12-16  Mathayo 27:19

🔶 Ndoto unazoziota kila siku ukiwa umelala zinagusa mfumo wako wa maisha ya kila siku kutokana na kile kinachoendelea katika ndoto zako, na kuna watu wengi sana ambao maisha yao yamefungwa na kuharibiwa kutokana na ndoto walizowahi kuziota na kushindwa kuomba mbele za Mungu baada ya kuota hizo ndoto. Sikiliza kila ndoto unayoiota ukiwa umelala iwe unaikumbuka au huikumbuki au unaelewa maana yake au huelewi ujue kwamba ndoto hizo zinagusa maisha yako ya kila siku hivyo usijaribu kudharau na kupuuzia ndoto unazoziota kila siku.

❌ Je ndoto unazoziota kila siku zimehusikaje na maisha yako ya kila siku? Je hizo ndoto hazijaharibu maisha yako ya kila siku? Hakikisha kwamba unaombea sana mlango wako wa ndoto kila siku mbele za Mungu.

✔️ Kwa maelezo mengi kuhusu ndoto karibu ujipatie kitabu changu nilichoandika kiitwacho JINSI YA KUOMBEA MLANGO WAKO WA NDOTO ILI USITESEKE katika kitabu hiki nimeweka kanuni 13 za kuomba na utapokea maarifa makubwa sana, kitabu ni Tsh 5,000 ( Elfu tano ) wasiliana nami kwa maelezo zaidi.

( 7 ) Mfumo wangu wa maisha unaguswa na Watu wanaonizunguka kila siku.

Mhubiri 13:20; 18:24 Isaya 43:4

🔶 Watu wanaokuzunguka katika maisha yako na uliowaweka karibu nawe niwa msingi sana kuwachunga rohoni kwasababu watu wanaokuzunguka wanahusika sana kugusa mfumo wako wa maisha unayoishi ndio maana usipokuwa makini nanmwangalifu na watu wanaokuzunguka utajikuta maisha yako yanaharibika na tabia yako njema, hivyo hakikisha unamuomba Mungu akuongoze kuwa na watu sahihi wa kukuzunguka kila siku ya maisha yako kwasababu maisha yako yanahitaji watu ila sio kila mtu unatakiwa kumleta na kumweka karibu sana na maisha yako.

❌ Je wewe umezungukwa na watu wa aina gani? Hao watu wamebeba roho gani? Hakikisha unawaondoa watu wasiofaa waliokuzunguka na kumuomba Mungu akuunganishe na watu sahihi kwenye maisha yako kwaajili ya kusudi lako la maisha.

➡️ Kwa leo tunaishi hapa katika semina na siku ya kesho tutaendelea na mambo mengine yanayogusa maisha yako nakuomba kwa leo yafanyie kazi haya tuliyojifunza mpaka kesho tutakapoonana.

Kwa mawasiliano nami utanipata kwa namba hizi:

Vodacom +255 765 867574 ( WhatsApp ).

Airtel +255 785 855785

Tigo +255 673 784197

Kwa email address ni Pastorkibiriti@gmail.com

Mimi ni Mwalimu wa Neno la Mungu la Maarifa

Samwel Kibiriti.

Mei 16, 2021

Mbeya Tanzania.

@Kibiriti2021

Washirikishe watu wengine somo hili nao wapokee maarifa haya na tukutane siku ya kesho ya semina.




1 comment:

  1. Bwana Yesu kristo apewe sifa, umemfanyia kazi kubwa mtumishi wa Mungu. Mungu akukumbuke katika hili na iwe Kumbukumbu nzuri na kazi hii iwe baraka kwa wengi.

    ReplyDelete

Featured Post

JINSI MISINGI YA VIZAZI INAVYOWEZA KUKAMATA MAISHA YAKO.

Fahamu kwamba misingi ni chanzo au asili au chimbuko la mtu. Na msingi wako wa vizazi unatokana na ukoo wako na kabila lako.      ...