Semina ya siku 30 ( Christ For All People Church- Mbeya ).
KUYASHUGHULIKIA MALANGO YA KIROHO YANAYOGUSA MFUMO WAKO WA MAISHA YA KILA SIKU.
Msingi wa Semina.
Senior Pastor Samwel Kibiriti.
Mwanzo 1:1 Kumbukumbu la torati 28:52,55 Kutoka 12:23 Isaya 60:11 Maombolezo 4:12 Zaburi 24:7-10
Bwana Yesu Kristo asifiwe wana wa Mungu napenda kuwakaribisha katika Semina hii ya siku 30 inayolenga kuyashughulikia malango yako ya kiroho kwa njia ya maombi mbele za Mungu.
LENGO LA SEMINA HII:
Semina hii iko na malengo makubwa mawili yaani
( i ) Lengo la kwanza la semina hii ni kuyashughulikia malango ya kiroho ambayo yanagusa maisha yako ya kila siku hapa duniani. Yapo malango mengi ambayo huyagusa maisha ya watu kila siku na kusababisha maisha yao yawe yalivyo leo.
( ii ) Lango la pilo la semina hii ni kushughulikia mfumo wa maisha yako. Maisha ya mwanadamu Mungu ameyaweka katika mfumo na huu mfumo wa maisha unaanzia mtu anapozaliwa hadi anapofariki ambapo kuna mambo mengi sana hujitokeza na kukutana nayo katika maisha yake. Sasa katika semina hii tutakuwa na maombi ya kushughulikia mfumo wako wa maisha ili uweze kuishi maisha ambayo Mungu amekupangia alipokuumba na kukuleta hapa duniani.
Day 1 ya Semina.
KUJIWEKA WAKFU KWA MUNGU KWAAJILI YA KUYASHUGHULIKIA MALANGO YA KIROHO YANAYOGUSA MAISHA YAKO.
Kutoka 32:29 Yohana 17:19
Katika siku hii ya kwanza ya semina nataka tujifunze jambo hili la kujiweka wakfu kwa Mungu unaposhughulikia malango ya kiroho. Kumbuka kwamba kabla hujaombea malango ya kiroho ya maisha yako hakikisha kwamba unajiweka kwanza wakfu kwa Mungu, usijaribu kupambana na malango ya kiroho bila kujiweka wakfu kwa Mungu kwanza, kwasababu vita vya malango ni halisi kabisa hivyo unatakiwa utii hii kanuni ya kujiweka wakfu kwa Mungu kwanza.
KWANINI UJIWEKE WAKFU UNAPOTAKA KUOMBEA MALANGO YA KIROHO?
Kuna sababu mbalimbali zinazokuhitaji kujiweka wakfu kwa Mungu kwanza kabla ya kushughulikia malango ya kiroho yanayogusa maisha yako nami nikuonyeshe sababu hizi hapa;
{ 1 } Unapojiweka wakfu kwa Mungu kuombea malango Mungu atahakikisha kwamba anakulinda ukiwa kwenye maombi.
Zaburi 121:7 1Petro 1:5
🔶 Unapojiweka wakfu kwa Mungu wakati unapofanya maombi ya malango Mungu atahakikisha kwamba anakulinda ili usiweze kupata madhara na mashambulizi kutoka kwenye roho mbalimbali zilizokaa kwenye hayo malango unayoyaombea ili kuyafungua maisha yako, hivyo kama unataka ulinzi wa Mungu ukiombea malango ni lazima ujiweke wakfu kwake Mungu.
{ 2 } Unapojiweka wakfu kwa Mungu kuombea malango utapokea maelekezo toka kwake Mungu kuhusu kuyaombea malango yaliyotumiwa kuyafunga maisha yako.
Mwanzo 35:1 Kutoka 12:1-51
🔶 Unapojiweka wakfu kwa Mungu katika kuombea malango ya kiroho utambue kwamba Mungu atakupatia maelekezo yake ya nini unatakiwa kuomba na kufanya katika malango ambayo yametumiwa kuyafunga maisha yako unayoishi. Kuna watu wengi sana maisha yao yamefungwa kwenye malango ya kiroho sasa ni vigumu wewe kuyatambua hayo malango ila unapojiweka wakfu kwa Mungu kuombea malango Mungu atakupatia maelekezo yake kupitia Roho wake na kukuongoza katika malango yaliyofunga maisha yako ili uyaombee sawasawa na mapenzi ya Mungu kwaajili ya maisha yako kufunguliwa.
{ 3 } Unapojiweka wakfu kwa Mungu kuombea malango maana yake unairuhusu madhabahu ya Mungu isimame pamoja nawe katika maombi yako.
Zaburi 43:4
🔶 Faida nyingine ukijiweka wakfu kwa Mungu kuombea malango ya kiroho maana yake unairuhusu madhabahu ya Mungu isimame pamoja nawe katika hayo maombi yako unayofanya kuyaombea malango ya kiroho na kuyafungua maisha yako. Hivyo hakikisha kwamba kabla hujaanza kufanya maombi ya kushughulikia malango ya kiroho ujiweke wakfu kwa Mungu ndipo baada ya hapo uanze kufanya hayo maombi ya kuombea malango yako ya kiroho.
KIRI MAOMBI HAYA YA KUJIWEKA WAKFU KWA MUNGU:
Mungu Baba kwa jina la Yesu Kristo ninatubu kwako dhambi zangu na makosa yangu niliyoyatenda katika maisha yangu ninakuomba unisamehe kwa damu ya Yesu Kristo.
Leo sawasawa na neno lako la Kutoka 32:29 ninakubali kwa moyo wangu kujiweka wakfu kwako katika madhabahu kwa damu ya Yesu Kristo ili ninapokuwa naombea malango haya ya kiroho Mungu unilinde na kunipatia maelekezo yako na madhabahu yako iweze kusimama pamoja nami kila siku ya maombi kwa jina la Yesu Kristo. Pia wote nitakaokuwa nawaombea kwenye haya maombi ya malango nawaweka wakfu kwenye madhabahu yako kwa damu ya Yesu Kristo Amen.
■ Hakikisha kwamba kila siku kabla hujaanza maombi yako ya malango ujiweke wakfu kwa Mungu ndipo baada ya hapo uombee malango hayo utakayoongozwa na Roho wa Mungu kuyaombea.
✔️ Kwa leo tunaishia hapa katika Semina tukutane siku ya kesho ya Pili ya semina, hakikisha unafanyia kazi somo la leo.
Kwa mawasiliano nami utanipata kwa namba hizi
Vodacom +255 765 867574 ( WhatsApp ).
Airtel +255 785 855785
Tigo +255 673 784197
Kwa email address ni Pastorkibiriti@gmail.com
Mimi ni Mwalimu wa Neno la Mungu la Maarifa
Samwel Kibiriti.
Mei 15, 2021
Mbeya Tanzania.
@Kibiriti2021
Washirikishe na wengine somo hili tukutane siku ya kesho ya pili ya semina.
No comments:
Post a Comment