Post Top Ad

Post Top Ad

Thursday, May 9, 2024

 Madhabahu ya Maarifa ya Neno la Mungu:

VITA YA UZAO KATI YA SHETANI NA MWANADAMU.

Mwanzo 3:15 Matendo 13:23 Yohana 19:30

Bwana Yesu Kristo asifiwe mwana wa Mungu napenda kukukaribisha katika somo hili naamini kwamba litakuwa msaada mkubwa sana maishani mwako.

( Sehemu ya Kwanza ).

🔶 Kuna vita kwenye ulimwengu wa roho kati ya Shetani na uzao wa mwanadamu na vita hii imesababisha madhara makubwa sana katika maisha ya wanadamu ndani ya uzao. Inawezekana maisha unayoyaishi sasa hivi yamekuwa hivyo sababu ya hii vita iliyopo kwenye uzao wenu, sasa katika somo hili leo na kesho tutaona sababu za kiroho zinazomfanya Shetani kupambana na uzao wako au uzao wenu kisha tutaona tunawezaje kuishinda hii vita maishani mwetu.

FAHAMU MAMBO YAFUATAYO.

Kuna mambo kadhaa ambayo nataka uweze kuyafahamu kuhusiana na vita hii ya uzao wako au uzao wenu na shetani.


JAMBO LA KWANZA:

Shetani anapoinua vita ya uzao ni kuhakikisha uzao wa mwanadamu haumwabudu na kumtumikia Mungu.

Mwanzo 1:26 Isaya 43:7 Yohana 4:23-24 Kumbukumbu 10:12 Mika 6:8

🔶 Mungu alimuumba mtu kwa mfano wake na sura yake ili aweze kumwabudu na kumtumikia hapa duniani ndio maana mtu aliumbwa katika utukufu wa Mungu na Bwana Yesu akasema kwamba Mungu anawatafuta wanadamu watakaomwabudu katika roho na kweli.

Lakini shetani anapoinua vita ya uzao lengo lake kubwa ni kuhakikisha uzao wa mwanadamu hauishi maisha ya kumwabudu na kumtumikia Mungu ndio maana leo hii ukitazama kwenye uzao wa wanadamu wengi hawamwabudu na kumtumikia Mungu aliye hai aliyewaumba na kuwaleta hapa duniani sababu hii ni vita iko kwenye ulimwengu wa roho katika uzao wao.

🔵 Kumbuka kwamba Mungu anakutaka uishi maisha ya kumwabudu na kumtumikia yeye peke yake hivyo pambana na kuishinda hii vita ya shetani kwenye uzao wenu inayokuzuia usiishi maisha ya kumwabudu na kumtumikia Mungu, tumia Damu ya Yesu na Jina la Yesu Kristo katika kuomba kwako.

Pia kama wewe ni mzazi hakikisha kwamba nyie wazazi na uzao wenu mnaishi maisha ya kumwabudu na kumtumikia Mungu siku zenu zote hapa duniani.

JAMBO LA PILI:

Shetani anapoinua vita ya uzao ni kuhakikisha uzao wa mwanadamu unatembea na kuishi kwenye laana sio Baraka.

Matendo 3:25 Mwanzo 22:18 Kumbukumbu 28:59

🔶 Mungu alipomuumba mtu alimuumba katika Baraka na Mungu alikusudia kwamba kila mwanadamu aliyemleta hapa duniani anaishi katika maisha ya baraka sio maisha ya laana.

Hii vita ya shetani na uzao wa mwanadamu lengo lake ni kuhakikisha uzao wa wanadamu unaishi kwenye laana sio baraka za Mungu ndio maana leo hii unaona katika uzao wa wanadamu wanaishi maisha ya laana na kuteseka sana kimaisha.

🟢 Hivyo hakikisha unaishinda hii vita ya uzao wenu inayokulazimisha kuishi maisha ya laana na kutembea katika laana badala ya kuishi katika baraka tumia Damu ya Yesu na Jina la Yesu Kristo kuishinda hii vita kwenye uzao wenu.

Wewe mzazi na uzao wako hakikisheni kwamba mnaishi katika maisha ya Baraka na kutembea katika Baraka za Mungu sio kukubali kuishi katika maisha ya laana.

JAMBO LA TATU:

Shetani anapoinua vita ya uzao ni kuhakikisha uzao wa mwanadamu haumiliki na kutawala kimaisha.

Mwanzo 12:7, 17:7-8, 22:17, 28:14

🔶 Kumbuka kwamba Mungu amemleta mwanadamu hapa duniani aishi maisha ya kumiliki na kutawala sio kuishi maisha ya kumilikiwa au kutawaliwa lakini shetani ndiye ambaye anasababisha kwenye uzao wa wanadamu waishi maisha ya kutawaliwa na kumilikiwa.

Leo hii ukifuatilia maisha ya wanadamu wengi katika uzao wanaishi maisha ya kutawaliwa na maadui pia wanamilikiwa na roho mbalimbali za giza huu sio mpango wa Mungu kabisa bali hii ni vita katika uzao wenu inayokutazimisha wewe usiishi kabisa maisha ya kumiliki wala usiishi kabisa maisha ya kutawala.

🟡 Unahitajika kuingia kwenye maombi kwa kutumia Damu ya Yesu na Jina la Yesu Kristo kupambana na hii vita na kuishi ya shetani kwenye uzao wenu ili sasa wewe uishi katika uhalisia wa maisha yako ya kumiliki na kutawala hapa duniani.

Mzazi hakikisha wewe na uzao wako mnaishi maisha ya kutawala na kumiliki kwasababu huu ndio mpango halisi wa Mungu aliyewaumba.

➡️ Umekuwa unajiuliza kila wakati kwanini kwenye uzao wenu mnaishi maisha hayo ya mateso na maisha magumu na maisha yasiyofaa nataka ujue kwamba hiyo ni vita kati ya Shetani na uzao wenu na wewe ni lazima ukubali kusimama kwenye ulimwengu wa roho kwa njia ya maombi na Neno la Mungu ili kuishinda hiyo vita.

Nimekuonyesha sababu hizo 3 za muhimu ingawa ziko nyingi ili usiendelee tu kulalamika na kulia bali utambue kwamba uko kwenye vita ya uzao wenu na shetani anahakikisha kila mtu wa uzao wenu anaishi katika maisha ambayo sio ya kwake yale Original ya Uumbaji wa Mungu, hivyo unahitajika kuomba sana.


☑️ Siku yetu ya kesho tunapoenda kuhitimisha somo hili nitakuonyesha namna ambayo tunapata ushindi huu wa vita ya shetani na uzao wetu kupitia Yesu Kristo. Hakikisha tunaungana tena pamoja katika darasa letu hili ndani ya madhabahu huu ya Maarifa ya Neno la Mungu siku ya kesho, ila leo hakikisha unalifanyia kazi somo hili.

🔶 Kwa mawasiliano nami kuhusu Ushauri wa kiroho na Maombezi tumia number hii ya Utumishi +255 765 867574 pia tumia number hii kama Chombo chako cha Sadaka mbele za Mungu kwaajili ya kueneza Ufalme wake pamoja nami kupitia Sadaka zako.

Mimi ni Mwalimu wa Neno la Mungu la Maarifa 

      Samwel Kibiriti.

April 29, 2024

Mang'ola Karatu Arusha.

Washirikishe wengine masomo haya kama unavyoyapokea toka kwenye madhabahu hii ili nao wapate Maarifa ya Neno la Mungu.

No comments:

Post a Comment

Featured Post

JINSI MISINGI YA VIZAZI INAVYOWEZA KUKAMATA MAISHA YAKO.

Fahamu kwamba misingi ni chanzo au asili au chimbuko la mtu. Na msingi wako wa vizazi unatokana na ukoo wako na kabila lako.      ...