Post Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, July 21, 2021

 Semina ya siku 30 ( Christ For All People Church- Mbeya ).

KUYASHUGHULIKIA MALANGO YA KIROHO YANAYOGUSA MFUMO WAKO WA MAISHA YA KILA SIKU.

          Day 12 ya semina.

Na Mwalimu Samwel Kibiriti.

Asifiwe Yesu Kristo wana wa Mungu karibuni katika semina ya siku ya leo, tunaendelea na lango la Nafsi hebu twende pamoja na leo tena.

KUSHUGHULIKIA LANGO LA NAFSI YAKO ( C ).

Baada ya kumaliza kukufundisha kuhusu Sababu ya vita katika nafsi yako na jana nikakufundisha kuhusu Kwanini nafsi yako inashambuliwa kwenye eneo la akili? Naamini umepata maarifa hapo naomba leo tuone eneo lingine kuhusu Nafsi yako unalotakiwa kulishughulikia.

KUVUNJA MITEGO ILIYOKAMATA NAFSI YAKO NA NAFSI ZENU:

Mithali 18:7 Kutoka 34:12 Zaburi 124:7 Yeremia 50:24  2Timotheo 2:26

Leo katika semina nahitaji kusema nawe kuhusiana na mitego iliyokamata nafsi yako na nafsi za watoto wako, wazazi wako na ndugu zako, nataka ufahamu kwamba kuna mitego ya kiroho ambayo inaweza kukamata nafsi za wanadamu na wengi sana nafsi zao zinashindwa kufanya kazi kama Mungu alivyoziumba kwasababu zimeshikiliwa kwenye mitego na wengi hawajaivunja hiyo mitego na kuzifungua nafsi zao.

NAFSI YAKO INAWEZA KUWA IMEKAMATWA NA MITEGO IFUATAYO:

Ngoja nikuonyeshe baadhi ya mitego ambayo inaweza kuwa imeikamata nafsi yako au nafsi zenu ili uhakikishe unaingia kwenye maombi rohoni kuivunja hiyo mitego kwenye nafsi na kuifungua ili iweze kuwa huru na kumuomba Mungu Nafsi yako irudi katika utendaji kazi wake kama ilivyoumbwa na Mungu.


MTEGO WA KWANZA:

( 1 ) Nafsi yangu inaweza kukamatwa na mtego wa kiapo/viapo.

Hesabu 30:2,9

🔵 Huu ni mtego ambao umezikamata nafsi za watu wengi kiroho na kusababisha hizo nafsi ziwe katika vifungo na mateso. Viapo ambavyo wewe umevifanya katika maisha au au vilivyofanyika katika maisha ya familia na uzao wenu kama hujavishughulikia na kuvivunja ni kwamba vimekamata nafsi yako na kuifunga, kwasababu Biblia inasema kiapo kinafunga nafsi. Na watu wengi kila siku wanaingia kwenye viapo vya maneno na damu na sadaka bila kujua madhara yake kumbe wanaziingiza nafsi zao kwenye mateso ambayo huonekana katika maisha yao ya kila siku.

❌Je nafsi yako haijakamatwa na viapo? Je nafsi za watoto wako hazijafungwa na viapo? Je nafsi za wazazi wako na mke wako au mume wako au ndugu zako hazijafungwa na viapo? Hakikisha unapata msaada wa kiroho wa kufunguliwa nafsi yako katika viapo vyote vilivyofunga nafsi yako au nafsi zenu iwe viapo vya maneno au viapo vilivyohusisha damu au sadaka maombi yanahitajika kuisaidia nafsi na kuifungua ili uishi maisha yako mazuri.


MTEGO WA PILI:

( 2 ) Nafsi yangu inaweza kukamatwa na mtego wa maneno ya kinywa changu niliyoyatamka.

Mithali 6:2; 16:26; 13:3

🔴 Maneno ya kinywa chako unayoyaongea kila siku au uliyoyaongea yanaweza kuwa yameifunga nafsi yako katika mtego huo wa maneno na wengi nafsi zao zimekamatwa hapa kwasababu kuna maneno wanayoongea bila kufikiri ambayo huwapelekea nafsi zao kuingia kwenye mtego wa kiroho. Biblia inasema umekamatwa kwa maneno ya kinywa chako, je ni maneno ya aina gani ambayo uliyazungumza na yakatumiwa kuifunga nafsi yako?

Unahitajika kuingia kwenye maombi ya kuifungua nafsi yako kwenye mtego wa maneno ulioikamata na kuifunga nafsi yako, hakikisha kwamba unatubu mbele za Mungu kuhusu maneno yote mabaya uliyojitamkia kwenye maisha yako kisha yafute kwenye ulimwengu wa roho na baada ya hapo ifungue nafsi yako kwenye hayo maneno, na uanze kujitamkia maneno mazuri na kuwatamkia maneno mazuri watoto wako. Hata kama unapitia wakati mgumu wa maisha yako chunga sana maneno unauoongea kwasababu yanakuwa na nguvu katika nafsi yako au katika nafsi ya huyo mtu unayemtamkia maneno hayo.


MTEGO WA TATU:

( 3 ) Nafsi yangu inaweza kukamatwa na mtego wa kuzimu.

Zaburi 16:10 Ayubu 38:17  Zaburi 30:3; 49:15 Mithali 27:20 Zaburi 33:19

Ziko nafsi za watu wanaoishi hapa duniani lakini kiroho zimekamatwa katika mtego wa kuzimu na zinatumikishwa sana na roho za kuzimu kila siku na watu hao wameshindwa kutoka kwenye hiyo mitego ya kuzimu na mikono ya kuzimu hivyo kukuta maisha yao yamekuwa ya mateso kila siku kutokana na mambo yanayofanyika sirini kwenye nafsi zao. Biblia inaposema uitoe nafsi yangu mikononi kwa kuzimu maana yake ni uwazi kwamba unaweza kumuona mtu uko nae kumbe kiroho nafsi yake imeshikiliwa huko kuzimu na mambo mengi huendelea akiwa amelala kwenye ndoto anazoziota.

❌Je nafsi yako na nafsi zenu hazijashikiliwa kwenye mitego ya kuzimu na kuzifunga? Hakikisha kwamba unafanya maombi ya kuifungua nafsi yako na nafsi zenu na kuzitoa kwenye mikono ya kuzimu iliyozishikilia.


MTEGO WA NNE:

( 4 ) Nafsi yangu inaweza kukamatwa na mtego wa madhabahu za miungu.

Waamuzi 6:11-15, 25-26

Ziko nafsi za watu zimeshikiliwa katika mtego wa miungu mingine kama vile nafsi ya Gideon na familia na mji mzima zilikuwa zimefungwa kwenye ile madhabahu ya baali aliyokuwa nayo baba yake hadi Mungu alipompatia maelekezo kwamba akibomoe hiyo madhabahu ndipo nafsi zao zikafunguliwa. Kuna watu ambao nafsi zenu zimeshafungwa na wachawi na kishirikina katika madhabahu za miungu, na wengine zile madhabahu zilizomo ndani ya Familia zao na ukoo na makabila yao na nchi zao zimehusika kuzifunga na kuzishikilia nafsi zao.

❌Je nafsi yako au nafsi zenu hazijakamatwa na mtego wa madhabahu za miungu migeni? Unahitajika kupata msaada wa kuifungua na kuzifungua nafsi zenu kwenye hizo madhabahu za miungu na kuvunja vifungo vya hizo madhabahu kwenye nafsi zenu kisha kuiunganisha nafsi yako na madhabahu ya Mungu katika Yesu Kristo.


MTEGO WA TANO:

( 5 ) Nafsi yangu inaweza kukamatwa na mtego wa maagano ya miungu.

 Kutoka 20:3: 32:1-7; 23:32

Maagano ya miungu yametumika sana kiroho kuzikamata na kuzifunga nafsi za wanadamu wengi unaowaona wanaishi duniani pasipo wao kujua na kutambua. Kuna watu wanaishi maisha magumu naya kuhangaika kila siku kwasababu nafsi zao zimefungwa kwenye maagano ya miungu na hayo maagano hawajayavunja kwenye nafsi zao yameendelea kuzishikilia na kuzikamata nafsi zao. Kama umetokea kwenye familia na uzao ulioingia maagano na miungu nafsi yako inaweza kuwa imeshikiliwa hapo na unahitaji msaada wa kufunguliwa lakini pia wale wanaoenda au walioenda kwa waganga wa kienyeji nafsi zao zimefungwa huko hata kama walitubia hiyo dhambi.

Unahitajika kuingia kwenye maombi ya kuifungua nafsi yako na nafsi za watoto wako na wazazi wako na ndugu zako na mke na mume wako zilizofungwa katika maagano mbalimbali ya miungu migeni.


MTEGO WA SITA:

( 6 ) Nafsi yangu inaweza kukamatwa na mtego wa uzinzi/uasherati.

Mithali 6:26,32-33 1Kor 6:16-18

Huu mtego wa uzinzi na uasherati umezikamata nafsi za mamilion ya wanadamu duniani kutokana na wanadamu wengi kushiriki kwenye uzinzi na uasherati kila siku huku wao wakijifariji kwamba ni sharehe ya miili yao bila kutambua kwamba uzinzi/uasherati unafunga nafsi ya hao watu wanaoshiriki katika hizo ngono. Watu nafsi zao zimefungwa kwenye huo mtego na leo wamekuwa watumwa wa uzinzi na uasherati kwenye maisha yao na kujikuta wanaishi maisha ya mateso na majuto kwasababu ya uzinzi na uasherati waliofanya na wanaoufanya.

❌Je wewe nafsi yako haijafungwa katika mtego wa uzinzi na uasherati? Je nafsi za watoto wako na mke au mume wako na ndugu zako na wazazi wako hazijafungwa kwenye huu mtego wa uzinzi na uasherati? Achana na mambo ya uzinzi na uasherati kwasababu uko na madhara mengi sana kiroho katika maisha yako na moja ya madhara ni kwamba unaiharibu nafsi yako na kumbuka kuwa nafsi ndio iliyobeba maisha na mafanikio pia imebeba kiu ya kumtafuta Mungu n.k

Hakikisha unatafuta msaada kwa watumishi wa Mungu katika kufunguliwa kwa nafsi yako kwenye mtego wa uzinzi na uasherati kama unataka kuishi maisha yako uliyokusudiwa na Mungu lakini pia kama unataka kuishi maisha ya Amani na mafanikio.

🔶 Nimekuonyesha baadhi ya mitego hiyo ambayo kiroho imehusika kuzikamata nafsi za wanadamu wengi sana wanaoishi hapa duniani, je wewe ni mtego upi umeikamata nafsi yako au nafsi za watoto wako au ndugu zako? Unalojukumu kubwa la kwenda mbele za Mungu kwa maombi kuiombea nafsi yako na nafsi zenu ili upate msaada wake Mungu wa kufunguliwa na kuwekwa huru.

✔️ Leo semina yetu inaishia hapa hakikisha kwamba unalifanyia kazi somo hili mpaka siku ya kesho tutakapokutana tena katika semina nyingine. Nakuomba sana unisaidie kuwashirikisha watu wengine na magroup mengine somo hili ili Mungu pia awahudumie na kuwafungua kwenye maiaha yao.

Kesho nitakuonyesha lango lingine la kiroho la kushughulikia kweye maombi yako kwaajili ya maisha yako.

Kwa mawasiliano nami utanipata kwa namba hizi:

Vodacom +255 765 867574 ( WhatsApp ).

Airtel +255 785 855785.

Tigo +255 673 784197.

Kwa Email address ni Pastorkibiriti@gmail.com



Mimi ni Mwalimu wa Neno la Mungu la Maarifa

          Samwel Kibiriti.

Mei 26, 2021

@Kibiriti2021

Nikukumbushe kwamba tunaishi nyakati za mwisho na Yesu Kristo anarudi kulichukua kanisa hakikisha kwamba umeokoka kwa kumpokea Bwana Yesu na uishi maisha yanayompendezesha Mungu aliyekuumba kila siku hapa duniani.

No comments:

Post a Comment

Featured Post

JINSI MISINGI YA VIZAZI INAVYOWEZA KUKAMATA MAISHA YAKO.

Fahamu kwamba misingi ni chanzo au asili au chimbuko la mtu. Na msingi wako wa vizazi unatokana na ukoo wako na kabila lako.      ...