Semina ya siku 30 ( Christ For All People Church- Mbeya ).
KUYASHUGHULIKIA MALANGO YA KIROHO YANAYOGUSA MFUMO WAKO WA MAISHA YA KILA SIKU.
Day 13 ya semina.
Mwalimu Samwel Kibiriti.
Kristo Yesu asifiwe mwana wa Mungu karibu katika semina ya siku ya leo. Baada ya kumaliza kujifunza kuhusu kushughulikia lango la nafsi naamini kwamba umepokea maarifa mengi na kuombea nafsi yako, leo naomba nikupeleke katika lango lingine la kiroho unalotakiwa kuliombea.
KUSHUGHULIKIA LANGO LA UUMBAJI WAKO.
Mwanzo 1:26-27; 5:1-2
🔶 Katika ulimwengu wa roho kuna lango la uumbaji ambalo limebeba maisha yako unayoishi hapa duniani ya kila siku. Watu wengi hawana ufahamu wa kiroho kuhusu lango lao la uumbaji na hivyo kushindwa kufanya maombi kila siku kuombea malango yao ya uumbaji na hivyo kusababisha shetani na nguvu za giza kushikilia malango yao ya uumbaji na kuyatumia kuwatesa katika maisha yao na kuishi maisha magumu ya shida na taabu sana kinyume na mpango wa Mungu kuwaumba na kuwaleta hapa duniani.
KWANINI SHETANI ANAPAMBANA NA LANGO LA UUMBAJI LA MWANADAMU?.
Kuna sababu nyingi sana za kiroho zinazomfanya shetani apambane na wewe katika lango lako la uumbaji au apambane na watoto wako, wazazi wako, ndugu zako, au mke/mume wako katika lango lao la uumbaji, sasa nikiwa mwalimu wa Neno la Mungu la maarifa naomba nikuwekeee ndani ya moyo wako sababu chache hapa ili utambue uzito na umuhimu wa kuombea lango lako la uumbaji au kuombea malango ya uumbaji ya watu wanaokuhusu kila siku mbele za Mungu.
SABABU YA KWANZA:
( 1 ) Lango la uumbaji limebeba Kusudi lako la kuumbwa na Mungu.
Mwanzo 1:27 Warumi 9:11 Mithali 16:4 Matendo 13:36 Isaya 46:10
Lango lako la uumbaji ndilo limebeba kusudi lako la kuumbwa na Mungu hivyo shetani anapambana nawe katika lango lako la uumbaji ili usiweze kuishi hapa duniani ndani ya kusudi lako la kuumbwa na Mungu na mamilion ya wanadamu wengi waliopo hapa duniani hawajui kwanini Mungu aliwaumba na hivyo kushindwa kutambua kusudi lao la kuumbwa na kujikuta wanaishi maisha yaliyo nje ya kusudi la uumbaji wao.
Shetani na nguvu za giza wakifanikiwa kushikilia lango lako la uumbaji wewe utakuwa mateka wao hata kama hutaki kwasababu hawatakuruhusu uweze kuishi ndani ya kusudi lako la kuumbwa na Mungu na pia utakapojaribu kutafuta kusudi lako watakushambulia na kupambana na wewe sana. Kumbuka kuna madhara makubwa sana ya wewe kuishi nje ya kusudi lako la kuumbwa na Mungu kwasababu kusudi lako ndilo limebeba maisha yako na ule mkakati kamili wa Mungu kukuumba na kukuleta hapa duniani hivyo ukiishi nje ya kusudi lako ni mateso makubwa sana sana.
❌ Je katika lango lako la uumbaji hujabanwa na kuzuiliwa na shetani na nguvu za giza hapo ili usiweze kuishi ndani ya kusudi lako la kuumbwa na Mungu? Unahitaji msaada mkubwa wa maombi mbele za Mungu kufunguliwa kwa lango lako la uumbaji pia kufunguliwa kwa kusudi lako ili uweze kuishi ndani ya kusudi na kuyaishi maisha yako halisi ambayo Mungu amekupangia ndani ya kusudi lako la uumbaji.
SABABU YA PILI:
( 2 ) Lango la uumbaji limebeba viwango vyangu vya maisha niliyotakiwa na Mungu niyaishi.
Zaburi 37:7 3Yohana 1:2 Zaburi 1:3 Mwanzo 26:13 Waefeso 1:3-4
Lango lako la uumbaji limebeba viwango vyako vya maisha ambayo Mungu aliyekuumba alikukusudia kuweza kuyaishi hayo maisha, na shetani akitaka kukubana usiweze kuishi maisha yako uliyopangiwa na Mungu na kufikia vile viwango vya maisha mahali anapopambana nawe kiroho ni katika lango lako la uumbaji hapo ndipo vita inapovhezwa. Ndio maana leo watu wengi sana wanaishi maisha yasiyokuwa yao pia wako chini ya viwango vya maisha yao kwasababu wamezuiliwa hapo kwenye lango la uumbaji wasiweze kuyaishi maisha yao kwenye viwango vya Mungu aliyewaumba.
❌ Je wewe katika maisha yako hujazuiliwa kwenye lango lako la uumbaji usiweze kuishi katika viwango vya Mungu alivyokupangia kimaisha? Unahitajika kupata msaada zaidi wa kiroho kwenye hilo lango hakikisha unafanya maombi ya kuombea lango lako la uumbaji na kuyafungua maisha yako hapo kwa damu ya Yesu Kristo.
SABABU YA TATU:
( 3 ) Lango la uumbaji limebeba aina ya kazi ninayotakiwa kuifanya katika maisha yangu hapa duniani.
Zaburi 33:13-15; 104:23
🔵 Katika maisha yako hapa duniani Mungu hajakuleta ufanye kila aina ya kazi unayoiona au inayofanywa na watu wanaokuzunguka nataka ujitambue kwamba Mungu kila mtu aliyemuumba na kumleta hapa duniani kuna kazi maalum ambayo amemuandalia na kumkusudia kila mtu kuifanya kwaajili ufalme wake hapa duniani. Lakini mamilion ya wanadamu hata wewe wako nje ya kazi maalum ya uumbaji wao wanazofanya hapa duniani wengi hufanya kazi ambazo sio zile zilizomfanya Mungu amewaumba na kuwaleta hapa duniani wazifanye kila siku.
Lango lako la uumbaji linaposhikiliwa na shetani kiroho kati ya jambo lingine atakalokufanyia ni kuhakikisha kwamba kwenye maisha yako hapa duniani huishi kwa kuifanya kazi ile iliyokutoa mbinguni kwa Mungu bali atakuacha ufanye kazi nje ya kusudi lako la uumbaji pia atapambana nawe usitambue kabisa kazi uliyotumwa na Mungu kuifanya hapa duniani. Pamoja na kazi mbalimbali unazofanya nataka ujitambue kwamba kuna kazi maalum ambayo Mungu anakutaka hiyo uifanye kwa nguvu zako na muda wako mwingi kwasababu ndio iliyokufanya umeletwa hapa duniani na Mungu.
❌ Je wewe kazi unayoifanya hapa duniani ndio kazi maalum ambayo Mungu amekuleta uifanye kwenye maisha yako? Unahitajika kupata msaada wa kiroho mbele za Mungu kumuomba ili akusemeshe na kukuonyesha kazi aliyokutuma hapa duniani uweze kuifanya. Pia kuna watu wamefungwa katika lango la uumbaji ili wasifanye kazi ile iliyowaleta hapa duniani, hakikisha unaomba mbele za Mungu.
SABABU YA NNE:
( 4 ) Lango la uumbaji limebeba Mamlaka unayotakiwa kutembea nayo katika maisha yako hapa duniani.
Mathayo 28:18 Danieli 7:12
Lango lako la uumbaji pia limebeba mamlaka ya maisha yako unayotakiwa kutembea nayo hapa duniani katika ule wito wa Mungu aliokuleta hapa duniani ili uweze kuutumikia kwasababu kuna mazingira mengi hapa duniani naya kiroho ambayo yatapambana nawe na kukuzuia usiweze kutimiza wito wako ndio maana Mungu alipokuumba akakubebesha mamlaka yako maalum.
Lakini watu wengi wamepokonywa mamlaka zao au wengine wamefungwa wasiweze kutumia mamlaka zao na mambo hayo yamefanyika kwenye lango lao la uumbaji. Hivyo unatakiwa kuingia kwenye maombi na kumuomba Mungu katika lango lako la uumbaji na kumuomba Mungu akurejeshee mamlaka yako ya uumbaji kwaajili ya maisha yako hapa duniani.
➡️ Kwa leo tunaishia hapa kwenye semina yetu, nakuomba fanyia kazi somo la leo na kuingia kwenye maombi. Katika kitabu changu cha MAOMBI YA KUWEKA WAKFU KWA MUNGU MALANGO YA KIROHO YANAYOGUSA MAISHA YAKO nimeeleza lango la kazi za mikono ambapo nilifundisha madhara ya kufanya kazi ambayo sio Mungu amekutuma kuifanya hapa duniani. Pia kwenye kitabu changu cha VITU VILIVYOBEBWA NDANI YA KUSUDI LAKO LA KUUMBWA NA MUNGU nimeeleza kuhusu mambo mengi yaliyomo ndani ya kusudi lako la kuumbwa na Mungu, hakikisha kwamba unapata Nakala yako ya vitabu hivi na vitabu vingine nilivyokwisha kuandika ambavyo vimebeba Maarifa makubwa ya Mungu ya Neno la Mungu.
Kwa mawasiliano nami na kutoa sadaka zako kwenye madhabahu ya Mungu tumia namba hizi:
Vodacom M-pesa +255 765 867574 ( WhatsApp ).
Airtel Money +255 785 855785
Tigo Pesa +255 673 784197
Kwa Email address ni Pastorkibiriti@gmail.com
Mimi ni Mwalimu wa Neno la Mungu la Maarifa
Samwel Kibiriti.
Mei 27, 2021
@Kibiriti2021
Maisha yako hapa duniani yatakuwa ya faida kubwa sana kama utamwamini na kumtegemea Mungu katika kila jambo unalofanya kwenye maisha yako.
No comments:
Post a Comment