Post Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, February 28, 2017

10:22 PM

AINA TOFAUTI ZA MAOMBI.

AINA TOFAUTI ZA MAOMBI.




Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo karibu tena leo katika somo letu hili ili upokee maarifa.

KIPENGELE CHA SABA.

KUNA MAOMBI YA KUDAI HAKI ZAKO MBELE ZA MUNGU.

Huu ni mfumo mwingine wa maombi ambayo unaweza kuyafanya mbele za Mungu ambayo ni maombi ya kudai zile haki zako ambazo shetani na ufalme wake wamezizuia ili usiwe nazo.

   ziko haki zako nyingi sana ambazo kwenye ulimwengu wa roho shetani inawezekana kabisa amekuibia na kukufichia, ambazo sasa unatakiwa uanze kuzidai na kuzirudisha.

ngoja nikuonyeshe kwa mfano ili uweze kunielewa.

{ i } Uzima na Uponyaji ni haki yako kama ni mtoto wa Mungu, soma Yakobo 5:13-15, Isaya 53:5, 1Petro 2:24.

{ ii } Kuwa na Amani na furaha ni haki yako, soma Zaburi 122:7,8 119:165, Malaki 2:5

{ iii } Kuolewa na kuoa ni haki yako, soma Isaya 34:14, Mwanzo 2:18

{ iv } Kuzaa watoto kwenye ndoa yako ni haki yako, soma Kutoka 23:26, Zaburi 127:3

{ v } Kutokuharibika kwa mimba ni haki yako, soma Kutoka 23:26


{ vi } Kujifungua pasipo kufanyiwa operesheni ni haki yako, Soma Isaya 66:9

{ vii } Kufanikiwa kiuchumi ni haki yako, soma Waefeso 1:3, 2Wakorintho 8:9, Kumb 8:18


{ viii } Kuwa na ulinzi wa Mungu kila siku ni haki yako, soma 1Petro 1:5

{ ix } Kufanikiwa kibiashara ni haki yako, soma Isaya 48:17, Zaburi 32:8, Kumb 28:5,12

{ x } Kuishi maisha marefu ni haki yako, soma Ayubu 5:26, Kutoka 23:26, Zekaria 8:4  n.k

hizo ni baadhi tu ya haki zako ambazo Mungu anakutaka uzipate kwenye maisha yako wewe ukiwa kama mtoto wake.

je wewe unazo hizi haki zako kwenye maisha yako? au tayari shetani na ufalme wake wa giza wameshakunyanganya haki zako hizo? kama umeshapokonywa hizi haki zako na hauko nazo kwenye maisha yako ni lazima uingie kwenye maombi na kumuomba Mungu ili akurudishie hizo haki zako kwenye maisha yako.

kwa mawasiliano nami utanipata kwa;

 simu za mkononi ni

vodacom 0765 867574
Tigo   0673 784197
Airtel  0785 855785

kwa Email ni Pastorkibiriti@gmail.com



 

mimi ni mwalimu Samwel Kibiriti.


unaweza kujipatia kitabu chako cha somo hili la AINA TOFAUTI ZA MAOMBI kipo wasiliana nami kwa simu namba hizo au kwa Email hiyo, naweza pia kukutumia mahali popote pale ulipo duniani.

           @kibiriti 2017, Marchi 1 
9:31 PM

AINA TOFAUTI ZA MAOMBI.

AINA TOFAUTI ZA MAOMBI.




Shalom wana wa Mungu karibu sana ndani ya darasa kwa siku hii ya Leo. Naamini utapata maarifa Leo tena.


{ KIPENGELE CHA SITA }.

KUNA MAOMBI YA KUNG'OA KILICHOPANDWA NA SHETANI KWENYE MAISHA YAKO.

Haya ni maombi ambayo yanahusika na kung'oa vitu au mbegu za uovu zilizopandikizwa kwenye maisha yako na shetani na vitu hivyo hukutesa kwenye maisha yako.

Katika Ulimwengu wa roho upande wa giza kuna vitu vingi sana ambavyo havifai wanavyowapandikizia wanadamu kwenye miili yao na nafsi zao,

Unaweza kumkuta mtu amepandikiziwa roho mbalimbali mfano magonjwa, matatizo, mikosi, madeni, kushindwa, ulevi, uzinzi/uasherati, tabia mbaya n.k, hizi ni baadhi tu ya roho ambazo unaweza kupandikiziwa na zinakutesa sana sana kwenye maisha yako.

                                        MATHAYO 15

"13 Akajibu, akasema, kila pando asilolipanda Baba yangu wa mbinguni litang'olewa"
.
Unamuona Bwana Yesu anasema kwamba kila pando ambalo hajalipanda Baba yake wa mbinguni lazima ling'olewa, hii ikiwa na maana kwamba yako mapando ambayo yamepandikizwa na shetani ndani ya mtu, na yanatakiwa kung'olewa kwa njia ya maombi.

                                     MATHAYO 13

"25 Lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake".

Unaona kwamba shetani anaweza kupanda vitu vyake katikati ya maisha ya mwanadamu.

Ni kuulize wewe umepandikwa vitu gani maishani mwako na shetani? Au shetani amewapandikizia vitu gani watoto wako? Au amepandikiza nini kwenye familia na ukoo wenu?

Unaona kwamba unayokazi ya kumuomba Mungu na kung'oa chochote kile kilichopandikizwa ndani yako na shetani, wachawi, waganga wa kienyeji, roho za mizimu, maadui n.k

Kwa Leo naishia hapa tukutane siku ya kesho tena tukiendelea na somo hili.

Kwa mawasiliano nami utanipata kwa simu

Voda 0765 867574.

Tigo 0673 784197.

Airtel 0785 855785.


KAULI MBINU MWAKA 2017.

( 1 ) Acha dhambi.

( 2 ) Yesu Kristo anakuja.

( 3 ) Ishi katika maisha ya Utakatifu kila siku.





Mimi ni mwalimu Samwel Kibiriti Rafiki yako katika Kristo Yesu.


                                   @Kibiriti 2017, February 7.

Monday, February 6, 2017

9:01 AM

AINA TOFAUTI ZA MAOMBI.



        AINA TOFAUTI ZA MAOMBI.
               

Bwana Yesu Asifiwe Rafiki yangu katika Kristo Yesu. Karibu tena siku hii ya Leo ndani ya darasa hili la kupokoea Maarifa.

              { KIPENGELE CHA TANO }

Leo nataka tusongee mbele kidogo katika somo hili tuone Aina ya tano ya Maombi ambayo unatakiwa uyaombe.


KUNA MAOMBI YA KUMUULIZA MUNGU.


Huu ni mfumo mwingine wa maombi ambayo unatakiwa uyafanye mbele za Mungu, yaani unafanya maombi ya kumuuliza Mungu.

Wakristo wengi huwa hawafanyi maombi ya kumuuliza Mungu. Iko faida kubwa sana ya kufanya maombi ya mfumo huu wa kumuuliza Mungu
Ni kwanini ufanye maombi ya mfumo huu wa kumuuliza Mungu?

"Tunafanya maombi haya ya kumuuliza Mungu kwa sababu yako mambo mengi yasiyofaa yanayotuandama kwenye maisha yetu, ambapo hatujuia chanzo cha hayo matatizo au hayo mambo, sasa ni lazima tumwendee Mungu Baba kwa mfumo wa maombi haya kumuuliza kwamba Mungu ni kwanini kuna tatizo hili kwenye maisha yangu? Naye atakujibu na kukueleza chanzo chake."

Ngoja nikuonyeshe mifano ya watu wawili waliofanya maombi ya mfumo huu wa kuuliza,

                         Mfano wa Kwanza:

                               MWANZO 25

21 "Isaka akamwomba BWANA kwa ajili ya mke wake, maana alikuwa tasa. Naye BWANA akamwitikia, na Rebeka mkewe akachukua mimba".
22 "Watoto wakashindana tumboni mwake. Naye akasema, Ikiwa ni hivi, kuishi kwanifaa nini? Akaenda KUMWULIZA BWANA".
23 "BWANA akamwambia, Mataifa mawili yako tumboni mwako, Na kabila mbili za watu watafarakana tangu tumboni mwako. Kabila moja litakuwa hodari kuliko la pili, Na mkubwa atamtumikia mdogo".

Hapa unamuona Rebeka alipopatwa na shida ya mimba yake akaenda kumuuliza BWANA, yaani alifanya Maombi haya ya kumuuliza Mungu, na alimuuliza kwamba ni kwanini ile mimba inamsumbua. Na Mungu akamweleza sababu ya mimba hiyo kumsumbua na kumtesa.

Je wewe kuna jambo gani linalokutesa ambalo hujui chanzo cha tatizo hilo?

                          Mfano wa pili;

                          1 SAMWEL 23

2 "Basi Daudi akamwuliza BWANA, kusema, Je! Niende nikawapige hao Wafilisti? Naye BWANA akamwambia Daudi, Nenda ukawapige Wafilisti, na kuuokoa Keila".

Unamuona mfalme Daudi baada ya kuletewa taarifa kwamba Wafilisti wamevamia mji wa Keila na kuiba nafaka za watu, kabla hajaenda kupigana nao alichofanya Daudi ni kwenda Kumuuliza BWANA kwamba Je aende kupigana na Wafilisti au asiende? Na Mungu akamjibu na kumwambia aende kwa sababu atawashinda hao maadui zake.

Inawezekana na wewe iko vita kwenye maisha yako kwenye Ndoa, kazi, biashara, elimu, afya, uchumi, huduma n.k na huelewi chanzo cha hiyo vita sasa unachotakiwa ni wewe kwenda kwa mfumo huu wa maombi na kumuuliza Mungu kwamba "Ni kwanini vita hii imeinuka kwangu? Au kwanini napigana vita na Mimi sipati ushindi?" Ukimuuliza Mungu atakujibu na kukueleza chanzo cha hiyo vita na kukupatia mbinu za kuishinda hiyo vita.

Sijajua wakati unasoma somo hili uko katika hali gani ya kimaisha? Inawezekana yako mambo mengi sana ambayo yanakuandama kwenye maisha yako lakini hujui chanzo cha mambo hayo na umeomba lakini hujapata majibu kamili,

Sasa nakushauri katika Kristo Yesu nenda mbele za Mungu kwa mfumo wa maombi haya ya kumuuliza Mungu, kuhusu chanzo cha hayo matatizo hayo mambo hayo na Mungu atakujibu na kukueleza chanzo chake na atakupatia njia ya kufanya.
Kwa Leo naishia hapa tukutane siku ya kesho, fanyia kazi somo hili la Leo.

*                       Nataka nikueleze jambo hili kwamba mwisho wa wiki hii nitatoa kitabu cha somo hili la AINA TOFAUTI ZA MAOMBI ambapo nitaingia kwa undani sana, na kufundisha Aina nyingi sana za maombi ambayo unatakiwa uyafahamu na kumuomba Mungu."

Neema ya Mungu Baba ikuhifadhi.
Kwa mawasiliano nami utanipata kwa simu hizi

Voda 0765 867574
Tigo 0673 784197
Airtel 0785 855785

Asante sana kwa kujifunza somo hili.


mimi ni mwlm Samwel Kibiriti.

@Kibiriti 2017, February 6.

Saturday, February 4, 2017

2:33 AM

AINA TOFAUTI ZA MAOMBI

AINA TOFAUTI ZA MAOMBI.
 
Bwana Yesu asifiwe rafiki yangu katika Kristo Yesu, nakukaribisha tena siku hii ya leo ndani ya darasa la chuo hiki cha kupokea maarifa ya kiroho.
 
{ KIPENGELE CHA NNE }.
 
 Nataka tena siku ya leo tuangalie aina nyingine ya maombi ambayo unatakiwa kumuomba Mungu.
 
 
KUNA MAOMBI YA KINADHIRI.
 
Hii ni aina nyingine ya Maombi ambayo unatakiwa kumuomba Mungu na ukimwendea Mungu kwa mfumo wa maombi haya ya kinadhiri atakusikia na kutenda kwako sawa sawa na ulivyomuomba.
 
Maombi ya kinadhiri ni maombi ya jinsi gani?
 
Maombi ya kinadhiri ni maombi unayomuomba Mungu  kwamba akutendee jambo au akuvushe mahali hapo pagumu unapopitia kwenye maisha yako ambapo huoni msaada wowowte wa kutoka na unamuahidi Mungu kwamba ukinivusha hapa au ukinitendea hiki, mimi nitafanya kwako jambo fulani.
 
unapoenda mbele za Mungu kwa jinsi hiyo wewe kumuomba akuvushe mahali pagumu halafu akifanya hivyo na wewe utamtolea kitu fulani, nakuambia hivi Mungu Baba atakutendea kwa haraka sana hicho ulichomuomba kwa sababu anafahamu kwamba akikutendea wewe nawe kuna jambo utakalolifanya kwaajili yake Mungu.
 
ngoja nikupitishe kwenye mifano miwili tu ya watu ambao walienda mbele za Mungu kwa njia hii ya maombi ya kinadhiri na Mungu aliwajibu
 
{ 1 } Hana.
 
Hana alikuwa ni mke wa Elkana, na huyu mwanamke waliolewa wawili mwenzake alikuwa anaitwa Penina. Sasa huyu Hana alikuwa hana watoto lakini mwenzake alikuwa na watoto na kila siku Penina alikuwa anamdhihaki na kumsema vibaya Hana kwa sababu alikuwa ni tasa.
 
Biblia inasema siku moja baada ya Hana kumaliza kutoa sadaka huko Shilo akainuka na kukimbilia hekaluni kwa Mungu ambapo kuhani alikuwa ni mzee Eli, sasa angalia Hana alivyomuomba Mungu
 
1SAMWEL 1
10 Naye huyo mwanamke alikuwa na uchungu rohoni mwake, akamwomba BWANA, akalia sana.
 
11 Akaweka nadhiri, akasema, Ee BWANA wa majeshi, ikiwa wewe utaliangalia teso la mjakazi wako, na kunikumbuka, wala usinisahau mimi mjakazi wako, na kunipa mimi mjakazi wako mtoto mume, ndipo mimi nitakapompa BWANA huyo mtoto siku zote za maisha yake, wala wembe hautamfikilia kichwani kamwe.
 
12 Ikawa, hapo alipodumu kuomba mbele za BWANA, Eli akamwangalia kinywa chake.
 
17 Ndipo Eli akajibu, akasema, Enenda kwa amani, na Mungu wa Israeli akujalie haja yako uliyomwomba.
 
unamuona huyu mwanamke Hana anamwendea Mungu kwa mfumo huu wa maombi ya kinadhiri na anaweka nadhiri yake ya midomo kwa Mungu kwamba ampatie mtoto wa kiume na akamwambia Mungu kwamba akimpatia mtoto huyo atamtoa kwa Mungu na atakuwa mtumishi wa kutumika kwenye madhabahu yake maisha yake yote.
 
Sasa angalia alivyomuomba Mungu kwa maombi haya ya kinadhiri Mungu alifanya nini? je alimjibu maombi yake au hakumjibu?
 
1SAMWEL 1
 
20 Ikawa, wakati ulipowadia, Hana akachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; akamwita jina lake Samweli, akasema, Kwa kuwa nimemwomba kwa BWANA.
 
  Unamuona Mungu anayajibu maombi haya ya Hana ya kinadhiri aliyomuomba na kumpatia mtoto wa kiume sawa sawa na alivyomuomba Mungu.
 
Na baada ya Mungu kuyajibu maombi hayo ya Hana na kumtimizia alichomuomba unaona Hana naye anaitimiza ile nadhiri aliyomwekea Mungu "Naliomba nipewe mtoto huyu; BWANA akanipa dua yangu niliyomwomba; kwa sababu hiyo mimi nimempa BWANA mtoto huyu; wakati wote atakaokuwa hai amepewa BWANA. Naye akamwabudu BWANA huko" { mstari wa 27 na 28 }.
 
Sijajua na wewe unapolisoma somo hili uko katika hali gani ya kimaisha, Hana hakuwa na watoto na mke mwenzake alimdharau na kumbeza sana kila siku ikabidi aingie kwenye mfumo huu wa maombi ya kinadhiri, je wewe unasongwa na mambo gani kwenye maisha yako? usikate tamaa hebu mwendee Mungu kwa maombi kama haya ya kinadhiri na utaona jambo ambalo Mungu Baba atakutendea kwenye maisha yako.
 
{ 2 } Yakobo. 
 
Huyu ndugu Yakobo naye alimwendea Mungu kwa maombi haya ya kinadhiri ni kipindi ambacho alimkimbia kaka yake Esau ambaye alikuwa anamwinda ili amuue baada ya kuchukua mbaraka wake kutoka kwa baba yao Isack, ndipo mama yake Rebeka akamwambia Yakobo akimbie aende kwa mjomba wake Labani ili ajifiche huko kwanza ampaka zitulie hasira ya kaka yake.
 
Yakobo alipokimbia alikuwa hana kitu chochote kile na hata kule alikokua anaenda alikuwa hakufahamu, kwa ujumla alikuwa hana kabisa mwelekeo wa maisha hajui ataishije, atavaa nini, atakula nini n.k ndipo akamwendea Mungu aliye hai kwa maombi haya ya kinadhiri, angalia mistari hii,
 
MWANZO 28
 
20 Yakobo akaweka nadhiri akisema, Mungu akiwa pamoja nami, akinilinda katika njia niiendeayo, na kunipa chakula nile, na nguo nivae;
 
21 Nami nikirudi kwa amani nyumbani kwa baba yangu, ndipo BWANA atakuwa Mungu wangu.
 
22 Na jiwe hili nililolisimamisha kama nguzo litakuwa nyumba ya Mungu; na katika kila atakalonipa hakika nitakutolea wewe sehemu ya kumi.
 
Unayaona mazingira ya kimaisha aliyokuwa nayo Yakobo yalikuwa ni mabaya sana kwani alikuwa hana chakula cha kula, hana nguo, na matatizo mbalimbali akamwendea Mungu kwa maombi haya ya kinadhiri na Mungu akamjibu na kumtendea makuu mpaka alipokuwa anatoka nyumbani kwa huyo mjomba wake Labani huyu Yakobo alikuwa ni tajiri.
 
Sijajua na wewe mama yangu, baba yangu, kaka yangu, dada yangu, mdogo wangu na mtoto uko kwenye hali gani ya kimaisha inawezekana na wewe ni kama Yakobo huna chochote na hujui kabisa mwelekeo wa maisha yako utakuwaje umekata tamaa, nakuomba nenda mbele za Mungu kwa maombi kama haya ya kinadhiri.
 
Mweleze kabisa Mungu hali yako uliyonayo ya kimaisha usimfiche na mwambie kabisa kwamba Mungu nimefika mwisho nakuja kwako kwa maombi haya ya kinadhiri naweka nadhiri kwako kwamba ukinivusha kwenye haya maisha, matatizo, madeni, shida n.k mimi nitakutolea hiki/ nitakupatia hiki kama sadaka yangu ya nadhiri hii. ukishamuomba Mungu Baba hivyo utashangaa haraka sana anakujibu hayo maombi yako, ila kumbuka Mungu akishakutendea ni lazima na wewe ufanye ulichomwahidi kwa kukitoa sawa?
 
Naamini kwamba utafanyia kazi somo hili na utamwendea Mungu kwa mfumo wa maombi haya ya kinadhiri, Roho Mtakatifu akusaidie kuliingiza kwenye matendo ili uone baraka zake toka kwa Mungu.
 
Tukutane tena siku ya kesho ndani ya darsa hili la chuo hiki, wakaribishe na wengine.
Mkono wa Mungu Baba ukupiganie na kukushindia katika maisha yako.

KAULI MBIU MWAKA 2017.
  
{ 1 }  Acha dhambi
 
       { 2 } Yesu Kristo anakuja.
 
                                  { 3 } Ishi katika maisha ya utakatifu kila siku.
 
 Mimi ni mwalimu Samwel Kibiriti rafiki yako katika Kristo Yesu.
 
@Kibiriti 2017, February 4.
1:01 AM

AINA TOFAUTI ZA MAOMBI..

AINA TOFAUTI ZA MAOMBI. 


Shalom Rafiki yangu katika Kristo Yesu nakukaribisha tena siku hii ya Leo katika darasa letu hili la kupokea maarifa na kanuni hizi za kiroho.

{ KIPENGELE CHA TATU. }

Tunaendelea na aina nyingine ya maombi ambayo unaweza kuifanya, twende pamoja na Roho Mtakatifu akupatie uelewa na ufahamu, Katika kipengele hiki cha tatu.


KUNA MAOMBI YA KWENDA MBELE ZA MUNGU KWA KULIA.

Hii ni aina nyingine ya maombi ambayo unaweza kuyafanya mbele za Mungu yaani maombi ya kulia.

Unatakiwa uende mbele za Mungu kwa kulia, maombi haya ya kulia ni maombi ya pekee na yana mguso wa aina yake mbele za Mungu.

✔ Maombi haya ya kulia huingia kwenye moyo wa Mungu kwa kina na huleta majibu ya haraka kwa huyu anayeyaomba. Ni njia yenye majibu ya haraka.

Kwenda mbele za Mungu kwa Maombi ya kulia huonyesha Unyenyekevu na moyo uliopondeka mbele za Mungu, na kwamba huna tegemeo jingine yeye asipotokea na kukujibu.

✔ Kuna mazingira ambayo mwanadamu anaweza kufika ambapo akiangalia kila kitu haoni msaada wowote na hajui atatokaje katika mazingira kama hayo, saa nyingine unakuta kila mtu amekaa mbali nae hata marafiki na ndugu wamemuacha hajui afanye nini,  unachotakiwa ni kwenda mbele za Mungu kwa Maombi haya ya kulia, unamlilia Mungu na kumweleza kabisa kwamba Mungu ukinyamaza hapa Mimi naangamia, nakwambia Mungu hawezi kunyamaza na kuyaacha hayo machozi yako yaende bure Bali ataingilia kati maisha yako na kukutoa kwenye hayo mazingira magumu.

                       YEREMIA 31

"9 Watakuja kwa kulia, na kwa Maombi nitawaongoza; nitawaendesha penye mito ya maji, katika njia iliyonyoka; katika njia hiyo hawatajikwaa; maana Mimi ni baba wa Israeli, na Efraimu ni mzaliwa wa kwanza wangu".

Bwana anasema watakuja kwa kulia na kwa Maombi nitawaongoza, katika njia iliyonyooka, ambayo hawatajikwaa yaani hawatapata hasara.

Kwa hiyo hii ina maanisha nini? Pale ambapo huoni njia iliyonyooka kwenye maisha yako na hujui ataendaje mbele yako unachotakiwa nenda mbele za Mungu kwa Maombi haya ya kulia, naye anasema atakuongoza katika njia iliyonyooka.

Tujifunze kwa Hezekia alipokuwa ameumwa kiasi cha kufa alilia sana sana mbele za Mungu na Mungu akamjibu pale pale.

                           ISAYA 38

1 Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, BWANA asema hivi; Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona".

2 Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba BWANA",

3 akasema, Ee BWANA, kumbuka haya, nakusihi, kwamba nimekwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana"

4 Ikawa, neno la BWANA likamjia Isaya, kusema"

5 Enenda ukamwambie Hezekia, BWANA, Mungu wa Daudi, baba yako, asema hivi, Mimi nimeyasikia Maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitaziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano".

Huyu Hezekia alitakiwa afe na Nabii alishafika kuthibitisha kifo chake, lakini Hezekia kwa kwenda kwake mbele za Mungu kwa kulia, hukumu iligeuzwa pale pale na tamko jipya likatolewa la miaka yake kuongezwa zaidi.
       BWANA akamwambia Nabii Isaya nimesikia maombi yake, na nimeyaona Machozi yake, nitaongeza miaka yake. Machozi ni jibu la haraka toka kwa Mungu kwa ajili ya muhitaji wake.

✔ Hezekia alilia sana sana maana alikuwa hana namna nyingine ya kuishi, isipokuwa jibu la Mungu tu pekee.

Wako watu wanaofikili mtu anayemwendea BWANA kwa maombi ya kulia hana Imani huo ni utoto mchanga kiroho kuamini hivyo, maombi ya kulia mbele za Mungu yapo na Biblia imelieleza jambo hili kama nilivyokuonyesha hiyo mistari michache hapo juu.

Ukienda mbele za Mungu kwa Maombi ya kulia ni lazima atajifunua kwako na jibu la haja yako utalipata. Jitoe kwa Mungu katika maombi haya nawe utaona ushindi katika kila eneo la maisha yako.

Sifahamu muda huu unaposoma somo hili uko katika hali gani kimaisha? Inawezekana umebakia kama Hezekia huna namna ya kuishi magonjwa yanataka kukuua, madeni yamekuandama, hujui utawalisha nini watoto wako, biashara ni hasara tu, kazini wanatishia kukufukuza, kodi ya nyumba huna na kwenye nyumba anataka kukufukuza, unafeli sana kwenye masomo, Ndoa yako inataka kuvunyika n.k

Na wewe hujui ufanye nini umekata tamaa ya kuishi unaona kama vile Mungu amekutenga na kukuacha, naomba sikia Neno hilo tumaini lipo na Mungu Baba hajakusahau, hebu ingia kwenye maombi nenda mbele za Mungu kwa Maombi haya ya kulia mwambie Mungu aina msaada popote pale nimekata tamaa ya kuishi kutokana na haya yanayoniandama, lia sana mbele za Mungu na Mungu aliyemtokezea Hezekia atakutokezea na wewe na atayaona machozi yako naye atakuondoa katika hiyo shida na dhiki na mateso yako, naye atakuongoza katika njia iliyonyooka sawa sawa na mapenzi yake.

Kwa Leo naishia hapa tukutane tena siku ya kesho

 nitakapokuonyesha aina nyingine ya maombi. Fanyia kazi hili.

Kwa mawasiliano nami utanipata kwa simu


Voda 0765 867574
Tigo 0673 784197
Airtel 0785 855785


Mimi ni Mwalimu Samwel Kibiriti Rafiki yako atika Kristo Yesu


Neema ya Kristo Yesu iwe pamoja nanyi wote.

                   @kibiriti 2017, 3 February.
12:41 AM

AINA TOFAUTI ZA MAOMBI



AINA TOFAUTI ZA MAOMBI.

Bwana Yesu asifiwe Rafiki yangu katika Kristo Yesu karibu tena siku ya Leo ndani ya chuo chetu hiki cha maarifa ya kiroho, ili tupokee siri hizi.

{ KIPENGELE CHA PILI.}

Jana tuliangalia aina ya maombi ambayo ni maombi ya kulalamika naamini somo hilo la Jana limefanyika baraka kwako, na kama na wewe ulikuwa unaomba huku unalalamika najua kwamba umeshaanza kubadilika.

Tusongee mbele kidogo Leo tena.


KUNA MAOMBI YA KUOMBOLEZA.

Katika aina za maombi nataka ufahamu kwamba kuna maombi ya kuombeleza ambayo unaweza kuyafanya mbele za Mungu na Mungu akaingilia kati jambo hilo unaloliombea.

        YEREMIA 9

"17 BWANA wa majeshi asema hivi, Fikirini ninyi, mkawaite wanawake waombolezao, ili waje; mkatume na kuwaita wanawake wenye ustadi, ili waje;"

"18 na wafanye haraka na kutuombolezea, ili macho yetu yachuruzike machozi, na kope zetu zibubujuke maji".

Soma na mstari wa 20-21.

Tunamuona Mungu anawatafuta wanawake Waombolezaji ambao wanatakiwa wafanye haraka kuingia kwenye haya maombi ya kuomboleza na anasema pia wawafundishe na binti zao kuomboleza na kila jirani alie mbele zake kwasababu mauti imepandia kwenye nyumba zao.

     Kwahiyo unaona kwamba kuna jambo baya limeingia kwenye nyumba za hawa wanawake na Mungu anawataka waombe maombi ya kuomboleza kutokana na kile kitu kibaya kilichoingia ndani ya nyumba zao.

✔ Unaweza kumwendea Mungu kwa kufanya maombi haya ya kuomboleza kutokana na mambo ambayo ni chukizo unayoyaona ndani ya kanisa, ndani ya familia, ndani ya mji n.k

Sio tu kwamba wanawake ndio wanaotakiwa kufanya haya maombi ya kuomboleza hapana hata wanaume nao wanatakiwa kufanya maombi haya ndio maana Biblia ikasema "Na wafanye haraka na kutuombolezea, ili macho yetu yachuruzike machozi, na kope zetu zibubujike maji"
Kwahiyo tunahitaji kwenda mbele za Mungu kufanya maombi haya ya kuomboleza kutokana na maovu yanayoendelea kutendeka na tunayashuhudia kwa macho yetu na kuyasikia, hebu tuimimine mioyo yetu mbele za Mungu kwa kuomboleza na kumsihi Mungu asamehe haya yanayoendelea kwenye kanisa, familia, koo, miji, serikali n.k ambayo ni chukizo mbele za macho yake.

           YOELI 1

"13 Jikazeni mkaomboleze, enyi makuhani; Pigeni yowe, enyi wahudumu wa madhabahu; Njoni mlale usiku kucha katika magunia, Enyi wahudumu wa Mungu Wangu; Kwa kuwa sadaka ya unga na sadaka ya kinywaji Zimezuiwa katika nyumba ya Mungu wenu"

"14 ......iteni kusanyiko la dini, Wazee na wakusanye wenyeji wote wa nchi; Waende nyumbani kwa Bwana, Mungu wenu, Na kumlilia BWANA"

Naomba usome hiyo Yoeli Yote katika sura hii ya kwanza.

✔ Unamuona Mungu anazuia sadaka zisije kanisani na kuwataka makuhani yaani wachungaji na wahudumu wote wa madhabahu yake wafanye maombi haya ya kuomboleza na kulala usiku kucha kwenye madhabahu kwa sababu mvua ameizuia na matokeo yake wakulima wameshindwa kupanda na mifugo inakufa yenyewe kwa kukosa malisho.

Kwahiyo yako mambo ambayo yanatokea ambayo Mungu akiyatazama hayamfurahishi kabisa sasa nani wa kuyaombea? Ni Mimi na wewe twende mbele za Mungu tuomboleze na kumsihi asamehe huo uovu na dhambi anazozitazama, na tukiomba kwa Imani Mungu Baba atasamehe.

            YOELI 2
"12 Lakini hata sasa, asema BWANA, nirudieni Mimi kwa mioyo yenu Yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuombolea".

Hii ni aina ya Maombi ambayo Roho Mtakatifu anaweza kukuongoza kuyaomba haya maombi ya Kuomboleza na wewe ingia na kuomboleza mbele za Mungu na kumsihi asamehe na kuingilia kati jambo hilo, naye atakujibu.

 ➤ Tuwapate wapi Wanawake na Wanaume watakaoomboleza mbele za Mungu?

➤ Tuwapate wapi vijana wakiume na wakike watakaoomboleza mbele za Mungu?

Kwaajili ya kanisa, nchi, miji, familia, koo,? Wako wapi?

Roho Mtakatifu akuwezeshe kusimama mbele za Mungu kufanya maombi haya ya Kuomboleza mahali ulipo.

Kwa Leo naishia hapa tukutane tena siku ya kesho ambapo nitakuonyesha aina ya tatu ya Maombi.

Kwa mawasiliano nami utanipata kwa namba hizi

Vodacom 0765 867574.
Tigo 0673 784197.
Airtel 0785 855785.


KAULI MBIU MWAKA 2017

( 1 ) Acha dhambi.
( 2 ) Yesu Kristo anakuja.
( 3 ) Ishi katika maisha ya Utakatifu kila siku.

      

 Mimi ni Mwalimu Samwel Kibiriti Rafiki yako katika Kristo Yesu.

            @Kibiriti 2017, February 2.
12:18 AM

AINA TOFAUTI ZA MAOMBI.


     AINA TOFAUTI ZA MAOMBI.

SOMO LA KWANZA 2017


Bwana Yesu asifiwe Rafiki yangu katika Kristo Yesu.
Nakukaribisha sana ndani ya darasa hili la kupokea maarifa ya kiroho sawa sawa na vile ambavyo Roho Mtakatifu atatuongoza kujifunza
.
Naamini kwamba somo la kuomba au maombi umelisikia sana likifundishwa sana na watumishi wa Mungu maeneo mbalimbali.

Sasa Mimi katika SOMO hili limelenga mambo haya yafuatayo:

1 Kukuonyesha AINA tofauti tofauti za maombi.

2 Kutokana na wewe kuelewa hizi aina tofauti za maombi utabadilisha uelewa wako kuhusu maombi, kwa sababu inawezekana kuna makosa unayoyafanya kuhusu maombi.

3 Kupitia somo hili litakusaidia kupata majibu kutokana na kuomba kwako.

Kwahiyo fungua moyo wako ili Roho Mtakatifu aweze kusema nawe kupitia somo hili.
     Na somo hili nitaligawa kwenye vipengele tofauti tofauti, kwahiyo hakikisha kwamba unafuatilia kipengele kimoja baada ya kingine. Karibu twende pamoja.

{ KIPENGELE CHA KWANZA }


KUNA MAOMBI YA KULALAMIKA.

Katika aina tofauti za maombi nataka ufahamu kwamba kuna maombi ambayo unaweza kuyafanya lakini yakawa ni maombi ya kulalamika, yaani unaomba huku unalalamika.
     Wako watu wengi sana ambao wanajua kwamba wanaomba kumbe wanalalamika lakini hawaombi Bali wanamlalamikia Mungu.


HABAKUKI 1

1 Ufunuo aliouona Nabii Habakuki.

2 Ee BWANA, nilie hata lini, wewe usitake kusikia? Nakulilia kwa sababu ya udhalimu, ila hutaki kuokoa.

3 Mbona wanionyesha uovu, na kunitazamisha ukaidi? Maana uharibifu na udhalimu u mbele yangu; kuna ugomvi, na mashindano yatokea.

4 Kwa sababu hiyo sheria imelegea, wala hukumu haipatikani; kwa maana watu wabaya huwazunguka wenye haki; kwa sababu hiyo hukumu ikipatikana imepotoka.

Hii ni habari ya Nabii Habakuki unamuona analalamika sana kuhusu mji aliokuwa anaishi yako mambo mabaya yalikuwa yanaendelea ndani ya huo mji.
     Akajikuta badala ya kuomba na kumuomba Mungu akawa analalamika kutokana na mambo Yale aliyokuwa anayaona kwenye huo mji.

                       HABAKUKI 2

"1 Mimi nitasimama katika zamu yangu, nitajiweka juu ya mnara, nitaangalia ili nione atakaloniambia, na jinsi nitakavyojibu katika habari ya kulalamika kwangu".

Unamuona Nabii Habakuki akiweka wazi kwamba katika sura ya kwanza aliwekwa na Mungu katika zamu aombe kwaajili ya mji aliokuwamo lakini akawa analalamika badala ya kuomba, na Mungu alinyamaza kimya wakati analalamika hakumjibu.

     Na katika hii sura ya pili ya Habakuki ndio unaona sasa akaamua kusimama katika zamu yake na Kumuomba Mungu na akaacha kulalamika.

✔ Nataka nikuulize swali hili wewe Rafiki yangu Je wewe katika maombi unamuomba Mungu au unamlalamikia Mungu?
  Wengi sana hawaombi Bali wanalalamika.

Sikiliza Mungu anaweza kukuonyesha mambo ya udhalimu na uovu kwenye hilo eneo unaloishi, kufanyia kazi, au hapo unaposali kama alivyomuonyesha Habakuki, Je Ukiyaona mambo hayo unamuomba Mungu aingilie kati na kuondoa huo udhalimu, uovu, ugomvi, na kupatikana kwa haki kwenye huo mji au unalalamika unapoyaona mambo hayo?

✔ Je hayo mambo mabaya unayoyaona ndani ya familia yako na ukoo wako unamuomba Mungu ayaondoe au unalalamika kutokana na kuona mambo hayo?

Nakuomba badilisha mtazamo wako kuanzia sasa hivi kuhusu Maombi acha kulalamika Bali omba.

Acha kulalamika kwaajili ya mambo mabaya unayoyaona kwenye Nchi, serikali, kwenye familia yako/yenu, kwenye ukoo wenu, kwenye mji unaoishi na kufanyia kazi, kwenye shule unayosoma, kwenye kanisa/huduma, n.k
Acha kulalamika Bali ingia kwenye maombi na muombe Mungu abadilishe hayo unayoyaona na kuyasikia.

Tukutane siku ya kesho tukiangalia kipengele cha pili. Fanyia kazi kipengele hiki tulichojifunza.

Neema ya Kristo Yesu ikuongoze.

Kwa mawasiliano nami utanipata kwa namba hizi

Vodacom 0765 867574
Tigo 0673 784197
Airtel 0785 855785.



KAULI MBIU YA MWAKA 2017.

( 1 ) Acha dhambi.
( 2 ) Yesu Kristo anakuja.
( 3 ) Ishi katika maisha ya Utakatifu kila siku.

Mimi ni mwalimu Samwel Kibiriti Rafiki yako katika Kristo Yesu.

           @2017, February 1
YOUR DESCRIPTION HERE
samwelkibiritiministry.blogspot.com|By Chuo Cha Maarifa ya Kiroho

Featured Post

JINSI MISINGI YA VIZAZI INAVYOWEZA KUKAMATA MAISHA YAKO.

Fahamu kwamba misingi ni chanzo au asili au chimbuko la mtu. Na msingi wako wa vizazi unatokana na ukoo wako na kabila lako.      ...